Dodoma FM

Sekondari ya Wotta kutatuliwa kero ya madawati

20 April 2021, 12:18 pm

Na; Selemani Kodima

Changamoto ya upungufu wa madawati katika shule ya Sekondari Wotta Wilayani Mpwapwa huenda ikapatiwa ufumbuzi baada ya kupatikana fedha za mfuko wa jimbo kiasi cha shilingi milioni moja na elfu thelathini na mbili.

Baadhi ya wananachi wakizungumza na Taswira ya Habari wamesema uhaba wa madawati ni jambo ambalo  limekuwa likiwaumiza kutokana na baadhi ya watoto kusoma wakiwa wamekaliwa madumu.

Raphael Samila ni Mkazi wa Mlunga amesema suala la uhaba wa madawati ni changamoto ya muda mrefu katika shule hiyo hivyo kutokana na ushirikishwaji wa wananchi  wanaamini litapatiwa ufumbuzi.

Kwa upande wake Diwani wa Kata ya Wotta Bw.Mugabe Athumani   amekiri kuwepo wa changamoto hiyo ambapo amesema wamechukua jukumu la kuwashirikisha wananchi na kuja na maamuzi ya kutengeneza madawati 51 ikiwa ni sehemu ya mahitaji ya sasa.

Pia amethibitisha kupokea fedha kutoka mfuko wa jimbo kiasi cha Shilingi Milioni moja na elfu thelathini na mbili ambazo zitaunganishwa na mbao kutoka kwa wananchi na ifikapo Mwezi Julai  mwaka huu wanatarajia kumaliza Changamoto hiyo.

Shule ya sekondari Wotta ni shule pekee ambayo imekuwa ikihudumia Kata mbili ikiwemo Wota na Wangi Tarafa ya Kibakwe Wilayani Mpwapwa.