Dodoma FM

Wakazi wa mkoa wa Dar es salaam waliopo katika migogoro ya ndoa, mirathi na talaka wanakaribia kupata suluhu

3 September 2021, 12:50 pm

Na;Mariam Matundu.

Inaelezwa kuwa Mkoa wa Dar es Salaam ni miongoni mwa Mikoa iliyogubikwa na mkinzano wa masuala ya kijamii ambapo tangu mwaka 2017 mashauri 7000 ya mirathi na mashauri 2000 ya migogoro ya ndoa yamefunguliwa.

Wananchi wa Mkoa wa huo walio katika migogoro ya Ndoa, mirathi na talaka wanakaribia kupata suluhu ya changamoto zao kwa wakati kufuatia kuanzishwa kwa kituo jumuishi kwa ajili ya huduma hiyo.

Hayo yamebainika leo wakati wa ziara ya Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii, Dkt. John Jingu wakati akikagua ukamilishaji wa kituo hicho, kilichopo Temeke Mkoani Dar es salaam kinachotarajiwa kutoa huduma kwa wakazi wa Wilaya zote za Mkoa huo.

Dkt Jingu amemshauri Mkuu wa Kituo hicho kuona uwezekano wa kutumia Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) katika utatuzi wa mashauri ya ndoa, mirathi na talaka ili haki ipatikane kwa haraka na kuondokana na mrundikano wa mashauri .

Naye Mkuu wa Kituo hicho, Jaji Zahra Maruma amesema kituo hicho kitawezesha kuharakishwa kwa usuluhishi na kesi zinazohusu ndoa, mirathi na talaka hivyo kuokoa muda wa kufanya shughuli nyingine za maendeleo.

Kwa upande wake, Jaji Mfawidhi wa Kituo hicho, Ilvin Mgeta amesema ziara ya Katibu Mkuu Dkt. Jingu Kituoni hapo ni hatua muhimu kutokana na dhamana anayoisimamia kupitia Wizara ya Afya, Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii hivyo itaongeza ushirikianao baina ya Wizara na kituo hicho ili kusadiana katika kutatua changamoto mbalimbali za utoaji wa huduma kwa wananchi

Ameeleza kuwa masuala yanayolengwa pia yanahusisha mustakabali wa watoto pamoja na Ustawi wa Jamii kwa ujumla wake hivyo Wizara yenye dhamana ina jukumu la kushirikiana na wadau wengine kuhakikisha huduma zinatolewa kwa ubora na haraka.