Dodoma FM

Wazee kuendelea kunufaika na sera ya matibabu bila malipo

15 April 2021, 1:34 pm

Na; Selemani Kodima.

Serikali imesema itaendelea kuwatambua wazee wenye umri wa miaka 60 na kuendelea  wasio na uwezo ili kunufaika na sera ya matibabu bila malipo.

Hayo yamesemwa leo bungeni na Naibu Waziri TAMISEMI Dkt Festo Dugange wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti maalumu  Gatti Zephania Chomete ambapo amesema ofisi ya Rais Tamisemi  inatekeleza  sera ya afya  ya mwaka 2007 na Sera ya Wazee ya mwaka 2003 inayoelekeza kutoa matibabu bila malipo kwa wazee wenye umri wa miaka 60 na kuendelea na wasio na uwezo kwa kuwatambua na kuwapatia huduma mbalimbali za afya.

Amesema Hadi December 2020 Jumla ya wazee Milioni Mbili laki tatu na arobaini na nne ,mia saba na arobaini na saba  wametambulika sawa na asilimia 80 ya makadirio ya wazee wote nchini.

Aidha akijibu swali la Nyongeza la mbunge Gatti ,Naibu Waziri Dkt  Dugange amesema  serikali imeendelea kuweka utaratibu kupitia mamlaka za serikali za mitaa na maafisa maendeleo ya  jamii kupita katika vijiji kwa kushirikiana na watendaji wa kijiji kuwatambua wazee wenye sifa na kuhakikisha wanapata Vitambulisho.

Amesema bado hawajafikia asilimia 100 kama ambavyo sera ya wazee inavyoanisha lakini jitihada za kufikia hapo zinaendelea .

Pamoja hayo Naibu waziri  wa TAMISEMI ametoa maelekezo kwa watendaji,wakurugenzi wa mamlaka za serikali kote nchini kuhakikisha wanaweka mpango kazi wakuwatambua wazee wote wenye umri wa miaka 60 na kuendelea wasiokuwa na uwezo kuweka mpango wa kuwapatia vitambulisho ili waweze kupatiwa matibabu bila malipo.