

8 August 2023, 4:46 pm
Ni muhimu kuwepo kwa upangaji na usimamizi wa bei elekezi katika shughuli mbalimbali za kibiashara, ili kuepusha migongano kati ya wafanyabiashara kutokana na kujipangia bei zao wenyewe na ushawishi binafsi kutoka kwa wateja.
Na Neema Shirima.
Baadhi ya Wafanyabiashara wa kokoto Jijini Dodoma wametoa pendekezo la kuwepo kwa umoja na usimamizi wa bei elekezi katika biashara hiyo, hii ni kwa sababu baadhi ya wafanyabiashara hao kukosa ushirikiano na kupanga bei zao wenyewe.
Akizungumza na Taswira ya Habari Bw. Mohamed Ramadhani mmoja wa wafanya biashara hao katika eneo la Mailimbili Darajani ametoa wito na kuwaomba wafanyabiashara wenzake kuwa na umoja katika shughuli hiyo na kuuza kwa bei elekezi bila kuangalia ushawishi wa wateja kwa wote wanaitegemea shughuli hiyo kujipatia kipato.
Aidha Bw. Isa Zuberi ambaye ni miongoni wamfanyabiashara katika eneo hilo amesema kuwa, sababu kubwa ya wafanyabiashara hao kutofautiana bei katika uuzaji wa kokoto, ni makubaliano binafsi kati ya mteja na mfanyabiaShara husika anayefikiwa na mteja licha ya kukiri kuwa bei waliyo kubaliana kuitumia katika eneo hilo ni Shilingi 2500 kwa ndoo moja huku akitoa ombi la kuwepo kwa vikao kati yao.
Kwa upande wake mmoja wa watengenezaji wa kokoto hizo Bw. Abdalah Issa amesema kuwa, kwao hali ni tofauti kwani malipo yao hufanyika kwa siku pale tu wanapo maliza shughuli ya kuponda kokoto kwa kiwango walicho kubaliana na mwajiri wake.