Dodoma FM

Huduma ya nishati ya Mafuta ya Petrol na Diesel yarejea

8 February 2023, 7:08 pm

Huduma hiyo sasa imerejea rasmi-Bahi.Picha na lango la habari

Ikiwa ni wiki la tatu tangu kituo cha Dodoma Fm kuripoti kuhusiana na adha ya kukosekana kwa huduma ya nishati ya Mafuta ya Petrol na Diesel kwa zaidi ya miezi mitatu katika kituo cha Princes Muro kituo pekee kinachotoa huduma hiyo katika makao makuu ya wilaya ya Bahi, huduma hiyo sasa imerejea rasmi.

Na Benard Magawa.

Akizungumza na kituo hiki Meneja wa kituo hicho Bwana Salimu Juma amesema kulitokea changamoto mbalimbali za kibiashara zilizosababisha huduma hiyo kusimama lakini kwa sasa kila kitu kimewekwa sawa hivyo huduma zimerejea rasmi.

“Amesema kituo hicho kitatoa huduma zote zilizokuwa zikitolewa hapo awali kwa muda wote wa saa 24 ili kuwaondolea wananchi wa Bahi kero ya kukosekana kwa mafuta iliyowatesa kwa muda wote ambao huduma hiyo haikuwepo.”

Bwana Salimu Juma.

Naye Bwana Lyimo Amiri Afisa Vipimo kutoka ofisi ya wakala wa vipimo Mkoa wa Dodoma ambaye alifika kukagua mashine za kuuzia mafuta kabla ya kituo hicho kuanza kazi amesema wameidhinisha huduna kutolewa baada ya kukagua mashine za kuuzia mafuta.

“Tumekagua na kujiridhisha na vipimo vitakavyotumika kupimia wateja mafuta katika kituo hiki, mashine zote nne tumezikagua zipo sawa hivyo tumeidhinisha huduma zianze kutolewa.”

Alisema Amiri.

Bwana Lyimo Amiri Afisa Vipimo.

Kukosekana kwa huduma katika kituo hiki kulisababishausumbufu mkubwa kwa wanachi wa Bahi ambao walilazimika kupata huduma kwa wachuuzi wa mafuta wilayani humo ambao wamekuwa wakitoa huduma kwa bei ya shilingi 3500/= kwa lita moja bei ambayo ililalamikiwa na watumiaji wa vyombo vya moto.