Dodoma FM

Rais wa Zanzibar Dkt.Alli Mwinyi amuapisha makamu wa kwanza wa Rais

8 December 2020, 3:14 pm

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akimkabidhi Hati ya Kiapo Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe.Maalim Seif Sharif Hamad, baada ya kumuapisha hafla hiyo iliofanyika katika ukumbi wa Ikulu Zanzibar leo 8/12/2020.(Picha na Ikulu)  

Na Pius Jayunga.

Rais wa Zanzibar na mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dr.Hussen Ali Mwinyi amemwapisha makamu wa kwanza wa Rais Mh.Maalimu Seif Sharif Hamad na kuwataka viongozi wa vyama vya siasa pamoja na wananchi kuunguna pamoja kuyaendeleza maridhiano.
Rais. Dr. Mwinyi amesema majukumu yote yaliyo ndani ya mamlaka yake atahakikisha anayatekeleza na tayari ameanza kwa kuwateua Mh. Nassoro Ahmed Mazrui pamoja na Mh. Omary Said Shaban kuwa miongoni mwa wajumbe wa baraza la wawakilishi wakitokea chama cha ACT-Wazalendo.

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk. Hussein Ali Mwinyi akiwa katika picha ya pamoja na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, baada ya kumalizika kwa hafla ya kuapishwa iliofanyika katika ukumbi wa Ikulu Zanzibar.(Picha na Ikulu)  

Aidha Rais Dr. Mwinyi amempongeza Mh. Maalimu Seif kwa kupendekezwa na chama chake kuwa makamu wa kwanza wa Rais wa Zanzibar na kwamba hatua hiyo inaonesha Imani kubwa waliyonayo wanachama wa ACT-Wazalendo juu ya kiongozi huyo.
Akizungumza baada ya kuapishwa, Makamu wa kwanza wa Rais katika Serikali ya awamu ya nane Zanzibar Mh. Maalimu seif Sharif Hamad amesema baada ya majadiliano ya kina ndani ya chama cha ACT-Wazalendo walikubaliana kwa pamoja kuwa tayari kufanya kazi na Serikali ya awamu ya 8 chini ya Rais Dr. Mwinyi kwa kutanguliza masilahi mapana ya Nchi.

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk. Hussein Ali Mwinyi akihutubia wakati wa hafla ya kumuapisha Makamu wa kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, hafla hiyo imefanyika leo 8/12/2020 katika ukumbi wa Ikulu Zanzibar.(Picha na Ikulu)

Shughuli ya kuapishwa kwa Makamu wa kwanza wa Rais wa Zanzibar imefanyika katika ikulu ya Zanzibar na hii ni mara ya pili kwa Mh. Maalimu Seif Sharif Hamad kushika wadhifa huo ambapo awamu ya kwanza ilikuwa mwaka 2010 hadi 2015 katika kipindi cha uongozi wa aliekuwa Rais wa Zanzibar Dr. Ali Mohamed Shein.