Dodoma FM

Ukosefu elimu juu ya umuhimu wa vyeti vya kuzaliwa changamoto kwa wazazi

21 May 2021, 1:50 pm

Na; Thadey Tesha

Ukosefu wa elimu juu ya umuhimu wa vyeti vya kuzaliwa umetajwa kama miongoni mwa sababu zinazowafanya wazazi wengi kutofuatilia upatikanaji wa vyeti hivyo.

Hayo yamebainishwa na baadhi ya wazazi jijini Dodoma wakati wakizungumza na Taswira ya Habari ambapo wamesema mara nyingi wamekuwa hawaoni umuhimu wake hadi pale vinapohitajika kwa ajili ya kupata huduma fulani.

Akizungumza na Dodoma Fm afisa mawasiliano kutoka wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini(RITA), Bw.Jaffary Malema, amesema wazazi wanapaswa kuhakikisha watoto wao wanapata vyeti hivyo kwani vimekuwa na umuhimu mkubwa wanapotaka huduma mbalimbali.

Aidha amewataka baadhi ya wazazi kuacha tabia ya kulalamikia kucheleweshwa kupata vyeti hivyo pindi wanapovifuatilia kwani suala la upatikanaji wake ni mchakato ambao unahitaji kupata taarifa sahihi za mtoto.

Cheti cha kuzaliwa ni moja ya nyaraka muhimu ambayo inaelezea taarifa mbalimbali za kuzaliwa kwa mtoto ambapo Usajili wa vizazi unasimamiwa na sheria ya uandikishaji vizazi na vifo,(sura 108 toleo la 2002).