Dodoma FM

Wananchi Ihumwa A waomba kutengewa eneo la kuhifadhi taka

7 November 2023, 5:13 pm

Hili linajiri baada ya kata ya Ihumwa kuwa na ongezeko la watu ambao wamechangia kuzalisha taka katika mitaa mbalimbali ya eneo hilo. Picha na Msumba news.

Hali hii inashangaza kuona mtaa huo ambao haupo mbali na ulipo mji wa serikali ukikosa mzabuni wa kukusanya takataka  na wananchi wakichoma takataka katika maeneo yao wakati sheria zipo na miongozo ya udhibiti na utunzaji wa mazingira .

Na Victor Chigwada.

Wananchi wa mtaa wa Ihumwa A wameiomba serikali ya mtaa huo  kuwatengea eneo la kuhifadhi takataka  ili kuepuka mfumo wa kila mmoja kukusanya taka eneo lolote.

Taswira ya Habari imezungumza na wananchi wa mtaa mmojawapo wa kata hiyo kufahamu ni hatua zipi wanatumia kuhakikisha mtaa wao unakuwa safi kila wakati.

Baadhi yao wamesema ni muhimu serikali za mitaa kutenga maeneo ya kuhifadhi takataka kwani njia mojawapo ya kuongeza hali ya Usafi katika maeneo yao.

Sauti za wananchi.

Aidha wamesema kuwa wamekuwa wakitumia Vikundi na Watu binafsi kubeba Takataka lakini changamoto imekuwa ni wapi taka hizo zinaenda kukusanywa ili kuepusha uchafuzi wa mazingira kwa wakati mwingine.

Vilevile wamesema kukosekana kwa eneo maalum la kukusanyia takataka imesababisha baadhi ya watu kutupa takakata kwenye Mitaro ya Maji na maeneo ya makazi ya watu.

Sauti za wananchi.
Picha ni taka zilizo zagaa kutokana na kukosekana eneo maalum la kuhifadhi taka hizo. Picha na Msumba news.

Taswira ya Habari imeutafuta Uongozi wa Mtaa wa Ihumwa A  kwa ajili ya kupata Ufafanuzi wa changamoto hiyo ambapo Mwenyekiti wa mtaa huo Bw. Wiliamu Njilimuyi amekiri kuwa mtaa huo hauna sehemu maalumu ya kukusanyia Takataka kutokana na eneo ambalo lilikuwa likitumika awali kusitishwa.

Mwenyekiti huyo amesema ni vema wananchi kuendelea kutunza takataka na wakati mwingine kuzichoma katika maeneo yao wakati serikali ya mtaa huo ikiendelea kusubiri mzabuni wa ukusanyaji wa Takataka apatikane.

Sauti ya Bw. Wiliamu Njilimuyi.

Ikumbukwe kuwa Ihumwa A ni moja ya mitaa inayopatikana katika Halmashauri ya jiji la Dodoma ambapo ndani ya Halmashauri hiyo kuna idara ya Mazingira ambapo jukumu lao mojawapo ni Kusimamia usafi na uhifadhi wa Mazingira katika maeneo yote ya mipaka ya Jiji la Dodoma ikiwemo udhibiti wa uchafuzi wa Mazingira katika makazi,viwandani, mahotelini, maeneo mbalimbali ya kibiashara.