Dodoma FM

Wakazi wa Mbabala waiomba serikali iwapatie Elimu ya kutosha juu ya chanjo ya uviko 19

14 October 2021, 12:10 pm

NA; Shani Nicolous.

Wananchi wa kijiji cha Mbabala kata ya Mbabala Wilaya ya Dodoma mjini wameiomba serikali kupitia wizara ya afya kuongeza Elimu vijijini juu ya chanjo ya Uviko 19.

Wakizungumza na Taswira ya habari wananchi hao wamesema kuwa uhaba wa elimu ya kutosha juu ya chanjo hiyo imekuwa sababu ya mwitikio mdogo katika uchanjaji.

Wamesema kuwa maneno yamekuwa mengi ya upotoshaji kuhusu chanjo hiyo hivyo ni vema serikali kuongeza nguvu ya utoaji elimu .

Wameongeza kuwa pamoja na uhaba wa elimu kijijini hapo lakini kuna baadhi wamepata chanjo hiyo huku wengine wakishikiria mila na desturi zao zinazo wafanya kutokuchanja hivyo wanakijiji hao wanahitaji elimu zaidi juu ya ugonjwa huo na chanjo.

Kwa upande wake mwenyekiti wa mtaa wa Mphusu Bw. Lucas Hosea Fumbi amesema kuwa mikutano mbalimbali na watalaamu wa Afya iliyo fanyika imesaidia kuongeza uelewa na mwitikio wa kuchanja ,hivyo kuna haja kuongeza kasi zaidi vijijini kwani kuna vijiji ambavyo watu wake kufika hata katika mikutano ya kijiji ni changamoto.

Wakati serikali ikiendelea na zoezi la utoaji chanjo kwa baadhi ya mazingira bado kuna baadhi ya maeneo ya vijiji ambayo elimu hiyo haijawafikia ipasavyo , hivyo serikali ina kila sababu kutafuta mbinu mpya kwaajili ya kufikisha elimu hiyo sehemu nyingi hasa vijijini.