Dodoma FM

Rais Magufuli ameacha alama njema kwa Taifa la Tanzania

24 March 2021, 9:09 am

Na ;Mariam Kasawa.

Waziri wa Nchi ofisi ya waziri mkuu, Sera,Bunge,ajira ,vijana na wenye ulemavu Bi. Jenista Mhagama amesema kamati iliyo pewa kazi ya  kufanya maandalizi yote ya mazishi imekamilisha maandalizi hayo na bado inaendelea kusimamia mambo mbalimbali.

Bi. Mhagama ameyasema hayo alipokuwa akimkaribisha waziri mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. Kassim Majaliwa  ambaye pia ni mwenyekiti wa kamati ya mazishi Kitaifa, amemuhakikishia kuwa viongozi wote , mawaziri pamoja na Makati Wakuu wametekeleza yale yote waliyokuwa wakiagizwa tangu kutokea msiba huu na wataendelea kutekeleza hadi watakapo kwenda kumpumzisha hayati Dkt John Magufuli machi 26 2021 pale Chato Mkoani Geita.

Amesema anawashukuru viongozi wote na timu nzima ya kanda ya ziwa kwa ushirikiano wao, pia ametoa shukrani kwa watu wa kanda ya  ziwa kwa kumkuza shujaa alieliongoza Taifa la Tanzania na kuliachia alama  iliyo njema.

Nae Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. Kassim Majaliwa akitoa salam kwa wakazi wa Jiji la Mwanza  kutoka kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mama Samia Suluhu amesema  rais anawaomba wananchi kuwa watulivu, kuendeleza mshikamano pamoja na kuliombea Taifa katika kipindi hiki cha msiba hadi hapo machi 26 atakapo pumzishwa katika nyumba yake ya milele.

Mh; Majaliwa amemuelezea Hayati rais Magufuli kuwa ameacha alama kwa Taifa la Tanzania kila mahali mijini na vijijini  na pia amesema Mwanza ilikuwa sehemu yake ya kihistoria aliishi katika Mkoa huo aliyafanya mambo mengi ya maendeleo katika mikoa hiyo ya kanda ya Ziwa.

Aidha amewataka wakazi wa jiji la Mwanza kujipanga katika barabara ambazo mwili huo utapita ili waweze kutoa heshima zao za mwisho.

Amewashukuru viongozi na kamati zote zilizo husika kuandaa tukio hilo katika Mikoa yote ambayo mwili wa Hayati Dkt Magufuli ulipita kwa maandalizi na mapokezi makubwa waliyo yafanya wakati wa Tukio hilo.

Safari ya kuelekea Chato mkoani Geita inaanza leo baada ya wakazi wa jiji la Mwanza kutoa heshima zao za mwisho ambapo mwili huo utapitishwa maeneo mbalimbali kabla ya kufikishwa nyumbani kwao Chato Mkoani Geita.