Dodoma FM

TIRA yawataka wamiliki wa bima kuzingatia vitu muhimu

28 May 2021, 12:41 pm

Na; SHANI NICOLOUS.

Mamlaka ya usimamizi wa bima Tanzania TIRA wametoa wito kwa wamiliki wa bima kuzingatia vitu muhimu vinavyohitajika wakati wakileta madai yao ili kupatiwa huduma sahihi itakayosaidia kutatua madai hayo.

Akizungumza na Dodoma fm Afisa mwandamizi wa bima Maneno Adamu aliyemuwakilisha meneja wa kanda ya kati amesema kuwa ni muhimu kuandika dai lako kwa maandishi na vitu vingine vyote pamoja na maelekezo kutoka polisi.

Ameongeza kuwa bima inasaidia hasa kulinda mali yako na hata kuondoa hasara ambayo ingetokea baada ya kupata janga lolote linaloweza kutokea katika chombo chako husika pia kurahisisha matibabu ambayo yangeshindikana kwa kukosa pesa kwa kipindi husika.

Dodoma fm imezungumza na baadhi ya wananchi jijini hapa ambao wamesema kuwa wanatambua umuhimu wa bima katika jamii, hivyo wanaziomba mamlaka zinazohusika na bima kuboresha na kuanzisha bima mbalimbali kwa vipindi tofauti kulingana na mahitaji ya watu.

Kutokana na biashara ya bima nchini kuwa chini ya usimamizi, Mamlaka inatoa wito kwa wananchi kutolalamika na kunung’unika tu pale wanapopatwa na matatizo ya kibima kwa kutokujua wapi pa kwenda kwani Mamlaka kupitia ofisi zake za makao makuu na za kanda iko tayari kusimamia haki za watanzania na wakata bima.