Dodoma FM

Viongozi wa kata watakiwa kushirikishwa ili kila eneo nchini lipate anuani ya makazi

30 September 2021, 12:59 pm

Na; Alfred Bulahya.

Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dkt.Ashatu Kijaji amewataka Mameya,Wenyeviti na Wakurugenzi kuwashirikisha madiwani,watendaji wa kata vijiji na mitaa ili kuhakikisha kila eneo nchini linakuwa na anwani ya makazi.

Amesema Wizara yake imejipanga kuhakikisha kuwa hadi kufikia mwaka 2025 huduma za anwani ya makazi ziwe zimefika katika kila eneo nchini.

Kauli hiyo ameitoa Jijini Dodoma wakati akifungua semina ya kujenga uelewa na kuhamasisha utekelezaji wa mfumo wa anwani za makazi yaani Postikodi kwa Mameya,Wenyeviti na Wakurugenzi wa Majiji na Halmashauri za Wilaya.

Amesema Wizara ya Habari imepewa sh.bilioni 45 kwa ajili ya uratibu wa kuweka anwani hizo huku Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) ikipewa zaidi ya Sh.Bilioni 100 na hivyo kuwataka viongozi hao kusafiri kwa pamoja kukamilisha kazi hiyo.

Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dk.Zainab Chaula, amesema wamejipanga ifikapo mwaka 2025 kuhakikisha kila nyumba inakuwa na namba yake.

Amesema Mamlaka za Serikali za Mitaa na wakurugenzi wamekuwa wakipewa bajeti maalumu, lakini utekelezaji wake ni wa kusuasua, ambapo ameipongeza Halmashauri ya Jiji la Mwanza kwa kufanya kazi kubwa mpaka sasa.
Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, TAMISEMI, Prof.Riziki Shemdoe, amesema wameandaa sheria ndogo zitakazotumiwa na Halmashauri, katika kusimamia utekelezaji wa mfumo huo wa anwani za makazi.

Amesema postikodi zote zimeandaliwa na kuingizwa kwenye kanzidata, na kwamba hadi sasa Halmashauri 21 zimejengewa uwezo juu ya maudhui ya mfumo huo.