Dodoma FM

Wabobezi wa masuala ya jinsia waagizwa kutambua ahadi za nchi

22 June 2023, 3:18 pm

Waziri wa maendeleo ya jamii Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima akiwa katika picha ya pamoja na wataalamu wabobezi wa masuala ya jinsia.Picha na Maendeleo ya jamii.

Programu hiyo ya kizazi chenye usawa itakayotekelezwa kwa miaka mitano (2021/22 – 2025/26).

Na Mariam Matundu.

Wataalamu wabobezi wa masuala ya jinsia wameagizwa kutambua masuala yaliyowekewa Ahadi za nchi katika Jukwaa la kizazi chenye Usawa (GEF) ili kutekeleza Programu ya Kizazi chenye Usawa kwa Ufanisi.

Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima ametoa maelekezo hayo mkoani Morogoro Juni 22, 2023, wakati akifungua mafunzo kwa wataalamu hao walioteuliwa kusimamia utekelezaji wa ahadi hizo, zilizotolewa na Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kutekeleza maazimio ya Mkutano wa Beijing kuelekea Kizazi chenye usawa.

Waziri Dkt. Gwajima amewataka Wataalamu hao kuratibu Afua zinazotekelezwa na sekta zao na kuzitolea taarifa kwa wakati ikiwa ni pamoja na kuwa na taarifa zenye athari chanya kwa sekta zao zitakazoonesha mazuri yaliyotekelezwa na kuimarisha mawasiliano miongoni mwao.

Waziri wa maendeleo ya jamii Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima akizungumza katika mkutani huo. Picha na Maendeleo ya jamii.

Amesema lengo ni kufikia Usawa wa Jinsia na Uwezeshaji Wanawake Kiuchumi. Hivyo mafunzo hayo yanawajengea uwezo kuhusu Programu, Uratibu na utekelezaji ili kutekeleza malengo na ahadi zilizotolewa na Rais Mhe. Dkt. Samia.

Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Wakili Amon Mpanju amewataka wataalamu hao kuhakikisha wakitoka kwenye mafunzo hayo wanakwenda kuwa chachu ya utekelezaji wa Programu hiyo.

Naye Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Care International lililowezesha mafunzo hayo, Prudence Masako amesema shirika hilo linaunga mkono jitihada za utekelezaji wa ahadi za nchi Rais Samia alipotoa ahadi hizo za kuhakikisha usawa wa kijinsia unafikiwa katika eneo la haki ya usawa wa kiuchumi.

Programu hiyo ya kizazi chenye usawa itakayotekelezwa kwa miaka mitano (2021/22 – 2025/26), inatokana na ahadi ya Rais Mhe. Dkt. Samia katika utekelezaji wa maazimio ya Mkutano wa Beijing, kwenye Jukwaa la Kizazi chenye usawa kwamba atahakikisha usawa wa kijinsia unafikiwa hasa katika eneo la Haki ya kiuchumi.