Dodoma FM

Wananchi watakiwa kujenga utamaduni wa kupima afya zao mara kwa mara

5 August 2026, 13:02

Ugonjwa wa kisukari ni miongoni mwa magonjwa yasiyoambukiza yanayoendelea kuongezeka nchini. Picha na mtandao

Kwa mujibu wa Utafiti wa Taifa wa STEPS 2023, uliofanywa na Wizara ya Afya kwa kushirikiana na Shirika la Afya Duniani (WHO), asilimia 2.9 ya Watanzania wenye umri wa miaka 18 hadi 69 wanaishi na ugonjwa wa kisukari, huku asilimia 3.4 wakiwa na kiwango cha sukari kilicho juu kuliko kawaida, hali inayowaweka katika hatari ya kupata ugonjwa huo. Takwimu hizo zinaonesha umuhimu wa kuimarisha uhamasishaji wa uchunguzi wa mapema na kuzingatia mtindo bora wa maisha.

Na Husna Munisi.

Wataalamu wa afya wameendelea kuhimiza wananchi kujenga utamaduni wa kupima afya mara kwa mara ili kubaini mapema magonjwa yasiyoambukiza, ikiwemo kisukari.

Ugonjwa wa kisukari ni miongoni mwa magonjwa yasiyoambukiza yanayoendelea kuongezeka nchini. Hata hivyo, bado kuna upungufu wa uelewa sahihi pamoja na imani potofu kuhusu aina, dalili na namna ya kujikinga na ugonjwa huo, hali inayosababisha baadhi ya wananchi kuchelewa kufika katika vituo vya afya kwa ajili ya uchunguzi na matibabu.

Daktari Albert Martine kutoka mkoani Shinyanga amezungumza na KM24 ambapo ameeleza aina za ugonjwa wa kisukari na namna zinavyotofautiana.

Aidha, Daktari Martine amefafanua dalili zinazoweza kumfanya mtu kutambua mapema uwezekano wa kuwa na kisukari, akisisitiza umuhimu wa kufanyiwa vipimo mapema ili kuanza matibabu kwa wakati na kuepuka madhara yanayoweza kujitokeza.

Kwa upande wao, baadhi ya wananchi wameeleza kama wana utaratibu wa kupima afya zao mara kwa mara na kutoa maoni yao kuhusu umuhimu wa uchunguzi wa mapema wa kisukari.

Wataalamu wa afya wanaeleza kuwa kisukari kinaweza kuzuilika na kudhibitiwa kwa kuzingatia mtindo bora wa maisha, ikiwa ni pamoja na kula lishe yenye afya, kufanya mazoezi ya mwili mara kwa mara, kudhibiti uzito uliopitiliza na kupima kiwango cha sukari kwenye damu kwa wakati.

Sauti na Husna Munisi.