TANROADS yatenga bilioni 40 kukabiliana na athari za El nino
24 September 2026, 16:22

Maandalizi hayo yanalenga kuhakikisha miundombinu ya barabara inaendelea kuwa salama na kupitika, pamoja na kupunguza madhara yanayoweza kusababishwa na mvua hizo, ikiwemo uharibifu wa barabara na madaraja.
Na Anwar Shabani.
Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) umetenga zaidi ya shilingi bilioni 40 kwa ajili ya kukabiliana na changamoto zinazoweza kujitokeza kutokana na mvua za El Niño, zinazotarajiwa kuanza mwezi Oktoba mwaka huu.
Akizungumza kuhusu maandalizi hayo, Mtendaji Mkuu wa TANROADS, Mhandisi Mohamed Besta, amesema fedha hizo tayari zimetengwa ili kuwezesha hatua za haraka kuchukuliwa endapo miundombinu ya barabara itaathiriwa na mvua hizo.
Aidha, Mhandisi Besta amesema kadri hali ya hewa inavyoendelea kubadilika, Bodi ya Mfuko wa Barabara kwa kushirikiana na Wizara ya Fedha itaendelea kufanya tathmini na kupanga hatua za kukabiliana na changamoto zinazoweza kujitokeza katika maeneo mbalimbali, hususan mikoa ya ukanda wa pwani na mashariki ambayo imekuwa ikikumbwa na athari za mvua kubwa.