Umbali wa mabweni Nkaiti Sekondari kikwazo kwa wanafunzi ujifunza
9 October 2026, 16:09

Wanafunzi wa Shule ya Sekondari Nkaiti, iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Babati mkoani Manyara, wanakabiliwa na changamoto ya kutembea umbali mrefu kutoka nyumbani hadi shuleni pamoja na ukosefu wa mabweni, hali inayowaathiri katika kupata muda wa kutosha wa kujisomea.
Na Hamis Kitana.
Kutokana na changamoto hiyo, Shirika la Karimu Foundation limeahidi kujenga mabweni katika shule hiyo ili kuboresha mazingira ya kujifunzia na kuwawezesha wanafunzi kupata huduma bora za malazi.
Ahadi hiyo imetolewa na Mkurugenzi wa Karimu Foundation, Shau Erro Ae, wakati wa mahafali ya kidato cha nne yaliyofanyika shuleni hapo, ambapo amewataka wazazi kushiriki katika ujenzi huo kwa kuchangia asilimia 10 ya gharama za mradi.
Amesema ushiriki wa wazazi ni muhimu katika kufanikisha mradi huo, ambao unalenga kupunguza changamoto za wanafunzi na kuboresha mazingira ya elimu shuleni hapo.
Katika hafla hiyo, Shau Erro Ae pia amekabidhi vifaa vya michezo, vikiwemo mipira sita kwa ajili ya wanafunzi, na kutoa motisha ya shilingi milioni moja kwa walimu wa shule hiyo kwa lengo la kutambua mchango wao na kuwahamasisha kuendelea kuboresha elimu.