Watoto saba wenye PSORIASIS waomba kusaidiwa kupata bima ya afya
20 November 2026, 15:33

Watoto saba wa familia moja katika Kata ya Maghang, wilayani Mbulu mkoani Manyara, wanaosumbuliwa na ugonjwa sugu wa ngozi wa Psoriasis, wameiomba Serikali pamoja na wadau mbalimbali kuwasaidia kupata bima ya afya na huduma za matibabu ili kupunguza changamoto wanazokabiliana nazo kutokana na ugonjwa huo.
Na Hamis Kitana.
Watoto hao wamesema ugonjwa huo umekuwa ukiwaathiri katika maisha yao ya kila siku, huku wakikabiliwa na changamoto za kupata matibabu ya uhakika kutokana na hali ya kifedha ya familia yao. Wametoa ombi hilo baada ya kutembelewa na Mwenyekiti wa Chama cha Wagonjwa wa Psoriasis Tanzania, katika ziara iliyoambatana na utoaji wa misaada ikiwemo mafuta maalumu ya ngozi, sabuni na vifaa vya shule.
Kwa upande wao, wazazi wa watoto hao wamesema mbali na gharama za matibabu, wamekuwa wakikabiliwa na changamoto ya unyanyapaa kutoka kwa baadhi ya watu katika jamii kutokana na hali ya ngozi za watoto wao. Wameiomba Serikali na wadau kuwasaidia kupata huduma za matibabu pamoja na kuimarisha elimu kwa jamii ili kuondoa mitazamo potofu kuhusu ugonjwa huo.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chama cha Wagonjwa wa Psoriasis Tanzania amewataka wadau mbalimbali kujitokeza kusaidia familia hiyo, akisisitiza umuhimu wa kuhakikisha watoto hao wanapata huduma za matibabu na mahitaji mengine yatakayoboresha maisha yao.
Uelewa mdogo kuhusu ugonjwa wa Psoriasis, hususan katika baadhi ya maeneo ya vijijini, umetajwa kuwa miongoni mwa sababu zinazochangia unyanyapaa dhidi ya watu wanaoishi na ugonjwa huo, huku baadhi ya watu wakiuhusisha na imani za kishirikina badala ya kuutambua kama changamoto ya kiafya inayohitaji uelewa sahihi, matibabu na msaada wa jamii.