Dodoma kujenga shule za ghorofa kukabiliana na ongezeko la wanafunzi 2028
3 November 2026, 17:04

Halmashauri ya Jiji la Dodoma imeanza maandalizi ya ujenzi wa shule mpya za ghorofa katika maeneo mbalimbali ili kukabiliana na ongezeko la wanafunzi wanaotarajiwa kujiunga na kidato cha kwanza mwaka 2028, kufuatia mabadiliko ya mfumo wa elimu yanayotarajiwa kuongeza mahitaji ya nafasi za shule.
Na Victor Chigwada.
Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Ali Haji Jabir Shekimweri, amesema zaidi ya wanafunzi 34,000 wanatarajiwa kuhitimu elimu ya msingi katika halmashauri hiyo, hali inayohitaji maandalizi ya mapema ya miundombinu ya elimu ili kuhakikisha wanafunzi wanapata nafasi za kuendelea na masomo.
Amesema miongoni mwa mikakati iliyowekwa ni kujenga shule mpya katika maeneo ya Chahwa na Kilimani Chilolo, ambazo zitakuwa na majengo ya ghorofa ili kuongeza uwezo wa kupokea wanafunzi.
Shekimweri amesema taratibu za ujenzi wa miundombinu hiyo zimeanza na zinatarajiwa kukamilika ifikapo mwezi Mei mwakani ili shule hizo ziweze kuanza kutumika kwa wakati.