Ulevi wa pombe watajwa kuchangia vitendo vya ukatili katika jamii
23 November 2026, 17:04

Jamii inapaswa kuelimishwa kuhusu madhara ya unywaji wa pombe kupita kiasi, huku akihimiza matumizi yenye kiasi na kutafuta njia salama za kukabiliana na msongo wa mawazo. Amesema hatua hizo zinaweza kusaidia kupunguza migogoro ya kifamilia na vitendo vya ukatili, hivyo kujenga jamii yenye amani, heshima na mahusiano bora.
Na Daniel Njau.
Unywaji wa pombe kupita kiasi umetajwa kuwa miongoni mwa sababu zinazoweza kuchangia vitendo vya ukatili wa kijinsia pamoja na migogoro katika familia na jamii. Hali hiyo inatajwa kuhusishwa na kupungua kwa uwezo wa baadhi ya watu kudhibiti hisia, kauli na matendo yao wanapokuwa wamelewa.
Baadhi ya wananchi waliozungumza na Taswira ya Habari wamesema kuwa dhana ya pombe kusaidia kupunguza msongo wa mawazo imewafanya baadhi ya watu kuanza kuitumia kupita kiasi.
Wamesema tabia hiyo inaweza kusababisha watu kujihusisha na vitendo visivyofaa, ikiwemo lugha za matusi, ugomvi na ukatili dhidi ya wengine.
Kwa upande wake, Bi. Janne Ndetabura, mshauri wa masuala ya malezi, amesema unywaji wa pombe kupita kiasi unaweza kuathiri uwezo wa mtu kujidhibiti na kufanya maamuzi sahihi. Ameeleza kuwa hali hiyo inaweza kumfanya mtu kutumia lugha zisizofaa, kutoa kauli za kuudhi na kuonesha tabia za ukatili anapowasiliana na watu wengine.