Dodoma kuandaa mkutano wa NGOs 2026, washiriki 3,500 kutarajiwa
23 November 2026, 16:48

Mikakati ya kuimarisha mchango wa mashirika yasiyo ya kiserikali katika utoaji wa huduma kwa jamii inatarajiwa kujadiliwa jijini Dodoma Novemba 28, mwaka huu, kupitia Mkutano wa Mwaka wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali 2026.
Na Anwary Shabani.
Mkutano huo unaoandaliwa na Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum kwa kushirikiana na Baraza la Taifa la Mashirika Yasiyo ya Kiserikali (NaCoNGO), unatarajiwa kuhudhuriwa na washiriki takribani 3,500, wakiwemo viongozi wa Serikali, wawakilishi wa sekta binafsi, mashirika yasiyo ya kiserikali na wadau wa maendeleo kutoka ndani na nje ya nchi.
Akizungumza kuhusu mkutano huo, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Mheshimiwa Rosemary Senyamule, amesema mkutano huo ni fursa muhimu kwa mkoa huo kiuchumi na kijamii. Ameeleza kuwa moja ya malengo yake ni kukusanya fedha kupitia Mfuko wa Pamoja wa Ruzuku kwa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali (NGOs), utakaosaidia mashirika hayo kuimarisha utoaji wa huduma kwa wananchi.
Mkutano huo wenye kaulimbiu isemayo “Fikra Mpya kuhusu Uendelevu wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali: Ubunifu, Ubia na Upatikanaji wa Rasilimali Fedha kupitia Vyanzo vya Ndani” unatarajiwa kufanyika katika Uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma, kuanzia saa 11:30 alfajiri hadi saa 1:30 asubuhi.