Dodoma FM

Makundi rika yachangia matumizi dawa za kulevya kwa vijana

28 October 2026, 17:43

Picha ni kijana mwenye uraibu wa kutumia madawa ya kulevya kwa kujidunga sindano. Picha na Mwananchi.

Kwa mujibu wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia dawa za kulevya na uhalifu (UNODC) zaidi ya WATU milioni 331 duniani wameingia katika utegemezi wa dawa zenye asili ya kulevya huku watu milioni 63 wakipata madhara huku nchini Tanzania watu zaidi ya 62,000 wakiripotiwa kutafuta huduma za uraibu.

Na Victor Chigwada.

Makundi rika na tabia ya kuiga mienendo ya watu wanaowazunguka vimetajwa kuwa miongoni mwa sababu zinazochangia baadhi ya vijana kujiingiza katika matumizi ya bangi, pombe kali na dawa nyingine za kulevya.

Baadhi ya vijana waliozungumza kuhusu changamoto hiyo wamesema kukaa vijiweni na kuiga tabia za marafiki, pamoja na athari za utandawazi, kunachangia kuongezeka kwa tabia zinazoweza kuwaweka katika hatari ya kutumia dawa za kulevya.

Afisa Maendeleo ya Jamii wa Kata ya Ng’hambaku, Wilaya ya Chamwino, Richard Kisubi, amesema vijana wanahitaji kupewa elimu na ushauri nasaha ili kuwakinga wale ambao bado hawajaanza kutumia dawa za kulevya na kuwasaidia wale ambao tayari wameathirika.

Amesisitiza umuhimu wa kuwafikisha vijana walioathirika katika vituo vinavyotoa huduma za ushauri nasaha na matibabu ya uraibu ili kuwasaidia kukabiliana na madhara ya matumizi ya dawa hizo.

Simulizi na Victor Chigwada.