Dodoma FM

Wodi ya watoto njiti yachangia kupunguza vifo vya watoto Mpwapwa

25 November 2026, 16:41

Picha ni mtoto mchanga alipe katika kitanda kwaajili ya kumalizia hatua ya ukuaji wake. Picha na UN News.

Huduma maalumu kwa watoto wanaozaliwa kabla ya wakati, maarufu kama watoto njiti, katika Hospitali ya Wilaya ya Mpwapwa mkoani Dodoma, zimetajwa kuchangia kupunguza vifo vya watoto hao kwa kuwapatia uangalizi na matibabu yanayohitajika kulingana na hali zao za kiafya.

Na Stephen Noel.

Wadi hiyo imekuwa msaada mkubwa kwa watoto wanaozaliwa kabla ya kufikisha muda wa kawaida wa ujauzito, ambao huhitaji uangalizi wa karibu wa wataalamu wa afya kutokana na changamoto mbalimbali zinazoweza kujitokeza baada ya kuzaliwa, ikiwemo matatizo ya kupumua na kushindwa kudhibiti joto la mwili.

Akizungumzia huduma hizo, Kaimu Muuguzi Mkuu wa Hospitali ya Wilaya ya Mpwapwa, Philemon Daat, amesema uwepo wa wadi maalumu kwa watoto njiti umeimarisha utoaji wa huduma za afya kwa watoto hao na kuongeza nafasi zao za kuendelea kuishi, kutokana na kupatiwa matibabu na uangalizi unaostahili.

Amesema huduma zinazotolewa katika wadi hiyo zinahusisha ufuatiliaji wa karibu wa hali za watoto pamoja na matibabu yanayozingatia mahitaji yao ya kiafya, hatua inayosaidia kukabiliana na changamoto zinazoweza kuhatarisha maisha yao katika siku za mwanzo baada ya kuzaliwa.

Kwa upande wake, Belita Kusaga, ambaye ni mmoja wa wanufaika wa huduma hiyo, amesema uwepo wa wadi hiyo umekuwa faraja na msaada mkubwa kwa wazazi wenye watoto wanaozaliwa kabla ya wakati, huku akihimiza kuendelea kuboresha huduma za afya ya mama na mtoto ili kuhakikisha watoto wachanga wanapata nafasi nzuri ya kukua na kuendelea kuishi.

Ripoti ya Stephen Noel.