Dodoma FM

Kituo cha afya Dabalo chaomba jenereta kuimarisha huduma

7 October 2026, 17:24

Picha ni jenereta linalotumikakusaidia shughuli wakati umeme umekatika. Picha na BYC Power.

Na Victor Chigwada.

Ukosefu wa umeme wa uhakika katika Kituo cha Afya Dabalo, Wilaya ya Chamwino mkoani Dodoma, umeelezwa kuwa unahatarisha utoaji wa baadhi ya huduma za afya, hususan pale inapohitajika kufanya upasuaji unaotegemea nishati ya umeme.

Hali hiyo ya ukosefu ya umeme inawalazimu watumiaji wa umeme katika shughuli ndogo za uzalishaji, ikiwemo uchomeleaji, mashine za kusaga na kukamua mafuta, kusitisha shughuli zao ili kuruhusu kituo hicho kutumia umeme wakati wa kutoa huduma kwa wagonjwa.

Baadhi ya wananchi wamesema changamoto hiyo inaweza kuongeza gharama kwa wagonjwa, kutokana na baadhi yao kupewa rufaa kwenda vituo au hospitali nyingine pale huduma inayohitaji umeme inaposhindikana kutolewa.

Wananchi wameiomba Serikali na wadau wa afya kusaidia upatikanaji wa jenereta la dharura katika kituo hicho, ili kuhakikisha huduma za afya zinaendelea bila kuathiri shughuli nyingine zinazotegemea umeme katika eneo hilo.

Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Dabalo, Omary Kiguna, amekiri kuwepo kwa changamoto hiyo na kusema inaathiri utoaji wa huduma katika kituo hicho kinachohudumia wananchi wa Dabalo pamoja na maeneo mengine ya jirani.

Kiguna amesema tayari ameiwasilisha changamoto hiyo katika Baraza la Madiwani, sambamba na kuwasiliana na Mganga Mkuu wa Wilaya, DMO, ili kutafuta namna ya kutumia mapato ya ndani katika kupata jenereta la dharura kwa kituo hicho.

Simulizi na Victory Chigwada.