Dodoma FM

Polisi Dodoma yakamata watuhumiwa 56 kwa makosa mbalimbali ya jinai

10 November 2026, 16:39

Picha ni mikono ya mtuhumiwa ikiashiria yupo chini ya uchunguzi wa jeshi la polisi. Picha na BBC Swahili.

Jeshi la Polisi Mkoa wa Dodoma limetoa wito kwa wananchi kuendelea kushirikiana na vyombo vya usalama kwa kutoa taarifa za uhalifu na vitendo vinavyotishia usalama wa jamii, ili kusaidia kudhibiti uhalifu na kulinda maisha na mali za wananchi.

Na Anwary Shabani.

Jeshi la Polisi Mkoa wa Dodoma limefanikiwa kuwakamata watuhumiwa 56 kwa makosa mbalimbali ya jinai, yakiwemo ubakaji, ujambazi wa kutumia silaha, vitisho vya kuua, mauaji na dawa za kulevya, kufuatia operesheni za kiusalama zilizofanyika kuanzia Oktoba 7 hadi Novemba 2026.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma, Afisa wa Polisi, ACP Gallus Hyera, amesema watuhumiwa hao wamekamatwa katika operesheni hizo ambazo zililenga kudhibiti uhalifu na kuimarisha usalama wa wananchi na mali zao.

Katika hatua nyingine, ACP Hyera amesema Jeshi la Polisi limebaini mtandao wa usafirishaji haramu wa binadamu baada ya kuwakamata watu waliokuwa wakisafirisha watoto na watu wenye ulemavu kutoka Bariadi mkoani Simiyu kwenda Dodoma kwa lengo la kuwatumikisha katika shughuli za kuombaomba.

Aidha, amesema Jeshi la Polisi limechukua hatua za kisheria dhidi ya watuhumiwa waliofikishwa mahakamani, huku likieleza mafanikio yaliyopatikana katika kudhibiti makosa ya barabarani kupitia operesheni hizo.

Simulizi na Anwary Shabani.