Dodoma FM

Wananchi Kibaoni walalamika kuzorota kwa huduma ya uzoaji taka

10 July 2026, 18:16

Licha ya kuwepo kwa mawakala wa ukusanyaji taka lakini taka zinaendelea kurundikana.Picha na Anwary Shaban.

Jiji ya Dodoma inakisiwa kuzalisha tani 350 za taka ngumu kwa siku ambapo kata za nje ya mji uzalishaji ni tani 114 na Kata za mjini huzalisha ni tani 236.

Na Anwary Shaban.

Wakazi wa mtaa wa Kibaoni kata ya Miyuji jijini Dodoma, wamelalamikia kuzorota kwa huduma ya ukusanyaji taka katika kaya zao na maeneo ya biashara.

Wakiongea na taswira ya habari wananchi hao wamesema  kero hiyo imekuwepo kwa muda mrefu licha ya kuwepo kwa mawakala wa ukusanyaji takalakini taka zinaendelea kurundikana na kupelekea hatari ya kuibuka kwa magonjwa ya mlipuko.

Wananchi hao wamesema ukusanyaji wa taka umekuwa wa kusuasua katika mtaa huo  hivyo wanaiomba mamlaka husika kuchukua hatua za haraka kurejesha huduma hiyo.

Kwa upande wake, Balozi wa Shina namba Nne, Zakayo Mbogoli, amesema pamoja na changamoto ya ukusanyaji  taka, bado baadhi ya wananchi wanachangia kuzorotesha usafi kwa kutupa taka ovyo na wengine kutumia usafiri wa bodaboda nyakati za usiku kutupa mafurushi ya taka kwenye maeneo ya wazi.

Taswira ya habari ilimtafuta mwenyekiti wa mtaa wa Miyuji Proper, Bw Hawadi Mbogela, ambapo amekiri kuwepo kwa changamoto hiyo ya mrundikano wa taka katika maeneo mbalimbali ya mtaa huo. Amesema tayari hatua zimeanza kuchukuliwa baada ya kupatikana kwa mzabuni mpya atakayesimamia ukusanyaji wa taka.

Anwary Kina

Jiji ya Dodoma inakisiwa kuzalisha tani 350 za taka ngumu kwa siku ambapo kata za nje ya mji uzalishaji ni tani 114 na Kata za mjini huzalisha ni tani 236.

Aidha wastani wa tani 150 tu ndiyo zinaondoshwa mjini kwa siku sawa na asilimia 66%, hali hiyo imekuwa ikichangiwa na uhaba mkubwa wa vifaa hasa Skip bucket .