Dodoma FM

Unyanyapaa kikwazo kwa wenye ulemavu wanaoishi na VVU

13 July 2026, 15:27

Picha ni Mkurugenzi wa Taasisi ya Foundation for Disabilities Hope (FDH), Michael Silali akiongea na waandishi wa habari.Picha na Anwary Shaban.

Kwa kuendelea kutoa elimu na kuondoa unyanyapaa, wadau wanaamini kampeni ya “Na Sisi Tupo” itasaidia kujenga jamii yenye usawa, inayowathamini watu wenye ulemavu wanaoishi na Virusi vya ikimwi  na kuwawezesha kuishi maisha yenye matumaini na heshima.

Na Anwary Shaban.

Unyanyapaa na mitazamo hasi kutoka kwa jamii umetajwa kuwa kikwazo kikubwa kinachowakabili watu wenye ulemavu wanaoishi na Virusi vya UKIMWI, hali inayochangia baadhi yao kushindwa kujitokeza kupata huduma na kushiriki kikamilifu katika shughuli za kijamii na maendeleo.

Hayo yameelezwa na Mkurugenzi wa Taasisi ya Foundation for Disabilities Hope (FDH), Michael Silali, alipokuwa akizungumza na Taswira ya Habari jijini Dodoma ambapo amesema mbali na changamoto ya maambukizi ya Virusi vya Ukimwi watu wenye ulemavu hukumbana na unyanyapaa, kutengwa na jamii pamoja na kukataliwa na baadhi ya familia zao kutokana na mitazamo potofu.

Silali amesema ili kukabiliana na changamoto hiyo, taasisi ya FDH imeanzisha kampeni ya “Na Sisi Tupo”, inayolenga kutoa elimu kwa jamii kuhusu haki za watu wenye ulemavu wanaoishi na Virusi vya ukimwi  kuondoa ubaguzi na kuhamasisha ushirikishwaji wao katika jamii.

Picha ni wajumbe walio hudhuria kikao hicho.Picha na Anwary Shaban.

Nao baadhi ya wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) wenye ulemavu mbalimbali, wakiwemo viziwi na wenye ualbino, wamesema bado kuna upungufu mkubwa wa elimu kuhusu maambukizi ya Virusi vya ukimwi  miongoni mwa watu wenye ulemavu. Wameeleza kuwa kampeni ya “Na Sisi Tupo” itasaidia kuongeza uelewa na kupunguza unyanyapaa unaowakabili.

Wanafunzi hao wameongeza kuwa baadhi ya watu wenye ulemavu wanapobainika kuwa wanaishi na Virusi vya ukimwi  hupoteza matumaini na kujiona hawana thamani kutokana na namna wanavyotengwa na jamii.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa FDH Michael Silali ametoa wito kwa jamii kuwapokea, kuwaheshimu na kuwapa huduma sawa watu wenye ulemavu wanaoishi na Virusi vya ukimwi , akisisitiza kuwa wao ni sehemu ya jamii na wanastahili haki, heshima na fursa sawa kama wananchi wengine.

Sauti ya kina Anwary.