Dodoma FM
Dodoma FM
29 April 2026, 17:18

Ili kuongeza kasi ya ukusanyaji, ofisi hiyo imeanza kuwafikia wadaiwa wakubwa 100 katika kila Halmashauri kupitia utoaji wa ankara na notisi, ambapo kundi hilo linachangia zaidi ya asilimia 89 ya deni lote mkoani.
Na Bennard Filbert.
Mkoa wa Dodoma unaendelea kuonyesha kasi ya kuridhisha katika ukusanyaji wa Kodi ya Pango la Ardhi baada ya kufikia asilimia 76.5 ya lengo lake, hatua inayotafsiriwa kama ishara chanya ya usimamizi imara wa sekta ya ardhi nchini.
Akizungumza na waandishi wa habari leo ofisini kwake, Kamishna Msaidizi wa Ardhi Mkoa wa Dodoma, Geofrey Mwamsojo, amesema hadi sasa jumla ya shilingi bilioni 17.5 zimekusanywa kati ya lengo la shilingi bilioni 23 kwa mwaka wa fedha 2025/2026.
Ameongeza kuwa kwa upande wa kitaifa, Wizara ya Ardhi ilipangiwa kukusanya shilingi bilioni 290, huku Kodi ya Pango la Ardhi ikiwa ni sehemu muhimu ya masharti ya umiliki wa ardhi kwa mujibu wa Sheria ya Ardhi, Sura ya 113.
Vilevile, kwa kushirikiana na TISEZA, juhudi zinaendelea kudai zaidi ya shilingi milioni 428.8 kutoka kwa wawekezaji, huku maeneo ya biashara kama vituo vya mafuta na viwanda yakipewa kipaumbele.
Kwa upande wake, Afisa Ardhi Mteule Mkoa wa Dodoma, Letare Shoo, ametoa wito kwa wadaiwa wote kulipa Kodi ya Pango la Ardhi ndani ya siku 14 tangu kupokea ankara. Ameonya kuwa hatua kali za kisheria zitachukuliwa, ikiwemo kufikishwa mahakamani na kufutiwa umiliki wa ardhi kwa watakaokiuka agizo hilo.