Unapambana vipi na mtindo mpya wa ndoa za utotoni (sogea tuishi)
30 June 2026, 17:49

Bado ipo haja ya kutafuta ufumbuzi zaidi kwenye suala la ukatili wa kijinsia hasa uwepo wa ndoa za utotoni, ambao umekuwa ukikatisha ndoto za watoto wa kike katika elimu na pia kuhataria afya zao.
Na Mariam Kasawa.
UTAFITI mpya wa kitaifa wa ukatili dhidi ya watoto na vijana mwaka 2024 ulionesha ukatili wa kingono, kihisia na kimwili kwa watoto umepungua ikilinganishwa na utafiti uliofanyika mwaka 2009.
Kwa mujibu wa utafiti huo mpya, ukatili wa kingono kwa watoto wa kike umepungua kutoka asilimia 33 hadi asilimia 11, kimwili ni kutoka asilimia 76 hadi asilimia 24 na kihisia kutoka asilimia 25 hadi asilimia 22.
Aidha, ukatili wa kingono kwa watoto wa kiume, umepungua kutoka asilimia 21 hadi asilimia tano, wa kimwili umepungua kutoka asilimia 74 hadi asilimia 21 na kihisia umepungua kutoka asilimia 31 hadi asilimia 16.
Matokeo ya utafiti huo yalitolewa na Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsi, Wanawake na Makundi Maalum, Dk. Dorothy Gwajima hivi kwamba ulifanyika kati ya Machi na Juni, 2024 na uliwafikia zaidi ya watoto 11,414 wenye umri wa miaka 13 hadi 24 kutoka mikoa yote 31 ya Tanzania Bara na Zanzibar.
Matokeo ya utafiti huu yataiwezesha serikali na wadau wake kuboresha na kuandaa mipango, programu na mikakati mbalimbali ya kutokomeza vitendo hiyo na kuimarisha ulinzi na usalama wa watoto na vijana kwa maslahi mapana ya kizazi cha sasa na kijacho.
Baadhi ya vyanzo vya ndoa hizo vimekuwa vikitajwa kuwa ni umaskini wa kipato na mila na desturi zilizopitwa na wakati ambavyo husababisha watoto wa kike kuingizwa kwenye ndoa.
Umri wa kuolewa, umekuwa ni miongoni mwa mambo yanajadiliwa kwa muda mrefu na watu wa kada mbalimbali katika vyombo vya habari na mitanadao ya kijamii, huku kukiwa na maoni yanayopingana.
Wapo baadhi ya watu ambao wanataka mtoto wa kike mwenye umri wa miaka 11 hadi 13 ambaye amevunja ungo, aruhusiwe kuolewa kwa amri ya mahakama, kwa kuzingatia vielelezo vya kimazingira ikiwamo afya.
Lakini pia wapo wengine ambao wanapendekeza Sheria ya Ndoa ya Mwaka 1971 ifanyiwe marekebisho hasa katika vifungu vya 13 na 17, kwa maelezo kuwa vinaruhusu mtoto wa miaka 15 aolewe kwa ridhaa ya wazazi.