Dodoma FM

Wadau wa mpira wa miguu Mpwapwa wamuita waziri wa michezo

23 July 2026, 16:36

Ni wakati sasa kwa uongozi wa Chama cha Mpira wa Miguu wilayani humo kuanzisha mashindano ya mara kwa mara yatakayosaidia kuibua vipaji.Picha na Mtandao.

Wameiambia Dodoma FM kuwa kwa muda mrefu wilaya hiyo imekosa mashindano ya mpira wa miguu,

Na Steven Noel.
Wananchi na wadau wa mpira wa miguu wilayani Mpwapwa wamemuomba Waziri mwenye dhamana ya Michezo kutembelea wilaya hiyo ili kukutana nao na kusikiliza changamoto zinazoikabili sekta ya michezo, kwa lengo la kutafuta suluhisho la kuendeleza michezo katika wilaya hiyo.

Baadhi ya wakazi wa Mpwapwa, akiwemo Emanuel Ndule, Nurah Mansour na Samson Kempanju, wameiambia Dodoma FM kuwa kwa muda mrefu wilaya hiyo imekosa mashindano ya mpira wa miguu, hali inayodhoofisha vipaji vya vijana na kushusha hamasa ya michezo.

Wamesema ni wakati sasa kwa uongozi wa Chama cha Mpira wa Miguu wilayani humo kuanzisha mashindano ya mara kwa mara yatakayosaidia kuibua vipaji na kurejesha ushindani wa soka.

Akizungumzia suala hilo, Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano wa Chama cha Mpira wa Miguu wilayani Mpwapwa, Thaniti Liembe, amekiri kutokuwepo kwa mashindano kwa sasa, lakini amesema mipango ya kuyaanzisha inaendelea ili kukuza na kuendeleza michezo wilayani humo.

Sauti ya wadau wa michezo.