Wananchi watakiwa kuchukua tahadhari dhidi ya utabiri wa hali ya hewa
14 September 2026, 15:20

Viongozi wa kata ya vighawe, wilaya ya mpwapwa, wameendelea kuhamasisha wananchi kujiandaa dhidi ya uwezekano wa mvua nyingi kwa kufuatilia taarifa rasmi za hali ya hewa, kutambua maeneo hatarishi na kuchukua hatua za kinga, huku wazazi na walezi wakitakiwa kuwaangalia watoto na jamii kutoa taarifa mapema kuhusu maeneo yanayoweza kuhatarisha usalama.
Na Stephen Noel.
Wananchi wa kata ya vighawe, wilaya ya mpwapwa, wametakiwa kuchukua tahadhari na kufanya maandalizi ya mapema kufuatia utabiri wa wataalamu unaoonesha uwezekano wa kuwepo kwa mvua nyingi katika kipindi kijacho, hali inayoweza kusababisha madhara kwa maisha na mali.
Wito huo umetolewa na viongozi wa kata hiyo, akiwemo diwani emanuel ndule, mtendaji wa kata na afisa elimu wa kata, ambao wamewataka wananchi kufuatilia taarifa rasmi za hali ya hewa na kuzitumia kama msingi wa kuchukua hatua za kinga badala ya kuzipuuza.
Diwani ndule amesema baadhi ya wananchi wamekuwa wakipuuza tahadhari zinazotolewa kuhusu uwezekano wa hali mbaya ya hewa, hivyo amewataka kuhakikisha maeneo yao ya makazi yako salama na kuepuka maeneo yanayoweza kuwa hatarishi wakati wa mvua.
Wazazi na walezi kuwaangalia watoto kwa karibu, huku wananchi wakishauriwa kutosafiri au kuvuka maeneo hatarishi pale usalama unapokuwa mashakani, pamoja na kushirikiana na serikali za mitaa kutoa taarifa mapema kuhusu maeneo yenye hatari ili hatua stahiki ziweze kuchukuliwa.