Dodoma FM

Mafunzo ya ujasiriamali yaongeza tija Bahi na Kondoa

30 September 2026, 16:52

Pichani ni baadhi ya wananchi wakipokea vifaranga hivyo kwaajili ya shughuli ya ufugaji ili kujikwamua kiuchumi. Picha na Anwary Shabani.

Mradi huo wa vifaranga unalenga kuwawezesha wananchi kutumia shughuli za kiuchumi zinazoweza kuwasaidia kuongeza kipato na wakati huo huo kukabiliana na changamoto zinazotokana na mabadiliko ya tabianchi.

Na Anwary Shabani.

Wajasiriamali katika Wilaya za Bahi na Kondoa mkoani Dodoma, wamesema mafunzo ya ujasiriamali na ufugaji wanayopata kupitia mradi wa kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi yamewasaidia kuongeza uelewa, kuboresha ufugaji na kuongeza tija katika shughuli zao za kiuchumi.

Wajasiriamali hao wameeleza hayo wakati wa zoezi la ugawaji wa vifaranga 2,100 vya kuku chotara kwa wanufaika wa mradi wa kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi unaotekelezwa na INADES Formation Tanzania kwa ufadhili wa Bread for the World.

Wamesema mafunzo hayo yamewasaidia kujifunza mbinu bora za ufugaji, ikiwemo namna ya kutunza kuku, kuwapatia lishe bora na kukabiliana na changamoto zinazoweza kujitokeza katika shughuli za ufugaji.

Picha ni vifaranga vilivyo tayari kwaajili ya kufugwa. Picha na Anwary Shabani.

Akizungumza wakati wa zoezi hilo, Daktari wa Mifugo kutoka INADES Formation Tanzania, Charles Bukula, amesema ugawaji wa vifaranga hivyo umefanyika baada ya wanufaika kupata mafunzo ya msingi kuhusu ufugaji bora, hatua inayolenga kuhakikisha wanapata matokeo chanya katika shughuli zao.

Picha ni Daktari wa Mifugo kutoka INADES Formation Tanzania, Charles Bukula, akitoa ufafanuzi zaidi kuhusu ufugajia bora. Picha na Anwary Shabani.

Bukula amesema INADES Formation Tanzania itaendelea kuwawezesha wanufaika kwa kuwapatia elimu na ushauri wa kitaalamu unaolenga kuongeza tija katika shughuli zao za kiuchumi, huku wakijengewa uwezo wa kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Simulizi na Anwary Shabani.