Dodoma FM

Mila potofu na ukatili wa kijinsia vyatajwa kukwamisha ndoto za mtoto wa kike

9 November 2026, 16:51

Picha ni mtoto aliyefanyiwa vitendo vya kikatili vinavyopelekea kukwamisha ndoto zake. Picha na Jamhuri media

Mila potofu na mitazamo hasi katika jamii vimetajwa kuwa miongoni mwa vikwazo vinavyoendelea kukwamisha ndoto na maendeleo ya mtoto wa kike, hasa katika maeneo ambayo bado yanaamini kuwa hatima ya mtoto wa kike ni kuolewa badala ya kupewa fursa ya kupata elimu na kujenga maisha yake ya baadaye.

Na Daniel Njau.

Wananchi wamesema wataendelea kuungana na kushirikiana katika kuhakikisha mtoto wa kike analindwa dhidi ya ndoa za utotoni, ukatili wa kijinsia na mila zinazoweza kudumaza maendeleo yake. Wameeleza kuwa ni muhimu wazazi, walezi na jamii kubadili mitazamo na kuweka mbele elimu pamoja na ustawi wa watoto ili kuwajengea mazingira bora ya kufikia ndoto zao.

Baadhi ya wananchi wamesema mila hizo pamoja na vitendo vya ukatili wa kijinsia vinawanyima watoto wa kike haki ya kujiendeleza na kutumia uwezo wao, huku wengine wakilazimika kukatisha masomo kutokana na ndoa za utotoni na shinikizo kutoka katika familia na jamii.

Wamesema kuwa mtoto wa kike anapaswa kupewa nafasi sawa ya kusoma, kukua na kutimiza malengo yake bila kubaguliwa kwa misingi ya jinsia.

Akizungumzia hali hiyo, mwanasheria Bi. Eddah Mariki amesema mtazamo unaochukulia ndoa kuwa ndiyo hatima ya mtoto wa kike unaweza kumkatisha masomo, kumnyima fursa za maendeleo na kumzuia kufikia malengo aliyokuwa amejiwekea.

Amesisitiza umuhimu wa jamii kutambua haki na uwezo wa mtoto wa kike, kumlinda dhidi ya mila potofu na ukatili wa kijinsia pamoja na kuhakikisha anapata nafasi ya elimu na kujenga mustakabali wake.

Simulizi na Daniel Njau.