Umeme watajwa daraja fursa maendeleo Manchali
12 November 2026, 16:50

Kwa mujibu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Serikali inalenga kuhakikisha kuwa ifikapo mwaka 2030 vitongoji vyote nchini Tanzania Bara vinakuwa vimefikiwa na huduma ya umeme kupitia miradi mbalimbali inayotekelezwa na kusimamiwa na wakala huo.
Na Victory Chigwada.
Wakazi wa Kijiji cha Manchali wamesema kufikishwa kwa huduma ya umeme katika vitongoji ambavyo bado havijafikiwa na nishati hiyo kutachochea maendeleo, kuongeza fursa za ajira na kurahisisha shughuli mbalimbali za kiuchumi na kijamii.
Wakizungumza na Taswira ya Habari, baadhi ya wananchi hao wamesema kukosekana kwa umeme katika vitongoji hivyo kumeendelea kuwa kikwazo kwa huduma na shughuli zinazotegemea nishati hiyo, hali inayowafanya washindwe kunufaika na fursa mbalimbali za maendeleo.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Manchali, Bw. Manyangalazi Manyangalazi, amesema licha ya huduma ya umeme kuwepo katika baadhi ya maeneo ya kijiji hicho, bado kuna vitongoji ambavyo havijafikiwa na huduma hiyo, hivyo kuhitaji jitihada zaidi za kuhakikisha wananchi wote wanapata nishati ya umeme.