Fahamu madhara ya kutokupima afya muda mrefu
18 August 2026, 17:03

Jamii inapaswa kutopuuzia dalili za kiafya, bali kufika kituo cha afya mapema kwa uchunguzi na ushauri wa kitaalamu ili kulinda afya zao.
Na Godson Haron.
Imeelezwa kuwa watu wanaoishi na dalili za kiafya kwa muda mrefu bila kwenda kupima afya wapo kwenye hatari ya kukabiliwa na madhara makubwa zaidi, ikiwemo kudhoofika kwa afya, kushindwa kufanya shughuli zao kwa ufanisi na kuongezeka kwa gharama za matibabu.
Hali hii inachangiwa na baadhi ya watu kupuuza dalili, kuamini zitaisha zenyewe au kutumia dawa bila kujua chanzo halisi cha tatizo, jambo linaloweza kuchelewesha kupata huduma sahihi.
Baadhi ya wananchi wa Mtaa wa Upendo katika kata ya mnadani wameeleza kuwa bado kuna watu wanaendelea kuishi na dalili kwa muda mrefu na kusubiri hali iwe mbaya ndipo waende kituo cha afya.
Mtaalamu wa afya Dkt. Alex Lazaro anasema kupuuza dalili zinazoendelea au kujirudia kunaweza kuchelewesha mtu kupata huduma inayofaa. anasema kuwa uchunguzi wa mapema humsaidia mtu kufahamu hali yake na kuchukua hatua kabla tatizo halijawa kubwa.