Vijana watakiwa kujenga uwezo wa kufanya maamuzi sahihi katika maisha
23 September 2026, 17:19

Kutowajengea vijana uwezo huo kunaweza kuwafanya kuiga au kufuata maisha ya wengine, huku akisisitiza kuwa wazazi, jamii na walezi wana wajibu wa kuwasaidia vijana kutambua lililo sahihi na kuwajengea uwezo wa kujitegemea.
Na Rahel.
Imeelezwa kuwa vijana wanapaswa kufundishwa namna ya kufanya maamuzi na kujisimamia wenyewe, ili waweze kutumia teknolojia kwa uangalifu na kuepuka athari zinazoweza kujitokeza.
Baadhi ya vijana wamesema ushauri kutoka kwa wazazi ni muhimu zaidi katika kipindi hiki cha maendeleo ya teknolojia, kwa kuwa wanakutana na taarifa na changamoto mbalimbali kupitia mitandao ya kijamii.
Wamesema mwongozo kutoka kwa wazazi unaweza kuwasaidia kuchambua mambo wanayokutana nayo, kuepuka madhara na kufanya maamuzi yatakayowasaidia kufikia mafanikio.
Kwa upande wao, wazazi wameeleza umuhimu wa vijana kuwa na utamaduni wa kuomba ushauri kabla ya kufanya maamuzi muhimu, wakisema uzoefu wa wazazi unaweza kuwasaidia kutambua changamoto na kuepuka makosa yanayoweza kujitokeza katika safari yao ya maisha.
Mshauri wa Malezi na Familia, Muhere Madam, amesema pamoja na vijana kuhitaji ushauri kutoka kwa wazazi, wanapaswa pia kufundishwa namna ya kufanya maamuzi na kujisimamia wenyewe.