Wazazi na jamii watakiwa kushirikiana kutoa elimu ya afya ya uzazi kwa watoto
26 October 2026, 17:13

Walimu na jamii wametakiwa kutoa elimu sahihi ya afya ya uzazi kwa watoto na vijana, huku wakisisitiza umuhimu wa wazazi kuondoa hofu ya kuzungumza na watoto wao kuhusu mabadiliko ya miili yao ili kuwajengea uelewa, maadili na uwezo wa kujilinda dhidi ya mimba za utotoni na magonjwa ya zinaa.
Na Daniel Njau.
Utandawazi umetajwa kuwa miongoni mwa sababu zinazochangia baadhi ya wazazi kushindwa kuzungumza na watoto wao kuhusu afya ya uzazi, hali inayoweza kuwafanya watoto kukosa uelewa wa mabadiliko ya miili yao na namna ya kujilinda.
Baadhi ya wananchi wamesema tofauti na miaka ya nyuma ambapo vijana walipata mafunzo ya mila na desturi kupitia jando na unyago, kwa sasa baadhi ya wazazi wamekuwa wakikwepa mazungumzo kuhusu afya ya uzazi, hivyo kuhitaji kuimarishwa kwa mawasiliano ya kifamilia.
Mtaalamu wa Afya na Mshauri wa Masuala ya Uzazi kutoka Trust Clinic, Bi Jamila Saidi, amesema watoto wanapaswa kupata elimu ya afya ya uzazi kuanzia umri wa miaka 12 hadi 15, kulingana na mahitaji yao. Amesema elimu hiyo huwasaidia kuelewa mabadiliko ya miili yao, kuzingatia maadili na kujilinda dhidi ya mimba za utotoni na magonjwa ya zinaa, akiwataka wazazi kuondoa hofu ya kuzungumza na watoto wao.
Wananchi hao wameeeleza mapendekezo yao kuimarisha ushirikiano kati ya baba, mama, walimu na wadau wengine katika kutoa elimu sahihi ya afya ya uzazi, badala ya kutegemea walimu pekee, ili kuwajengea watoto na vijana uelewa unaowawezesha kufanya maamuzi sahihi na kulinda afya zao.