Dodoma FM

Takwimu rasmi zatajwa kuwa msingi wa maamuzi ya maendeleo

18 November 2026, 16:54

Picha ni mfano wa taarifa za kitakwimu zinavyopaswa kuwa. Piacha na Timesmajira.

NBS imetakliwa kuendelea kushirikiana na taasisi nyingine katika kuweka viwango vinavyofanana vya takwimu, kuunganisha vyanzo vya takwimu pamoja na kuhamasisha mikoa kutumia takwimu rasmi katika kupanga mipango na kufanya maamuzi ya uwekezaji.

Na Anwary Shabani.

Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) imewataka wadau mbalimbali nchini, wakiwemo wizara, taasisi za umma na binafsi, vyuo vikuu pamoja na washirika wa maendeleo, kuimarisha ushirikiano katika uzalishaji, usambazaji na matumizi ya takwimu rasmi kwa ajili ya kupanga na kutekeleza mipango ya maendeleo.

Wito huo umetolewa na Mwenyekiti wa Bodi ya Usimamizi ya Ofisi ya Taifa ya Takwimu, Mhe. Anna Makinda, wakati wa kilele cha maadhimisho ya Siku ya Takwimu Afrika, akisisitiza kuwa ushirikiano kati ya NBS na wadau ni muhimu katika kuhakikisha takwimu zinazozalishwa zinakuwa na ubora na zinatumika ipasavyo katika maamuzi mbalimbali ya maendeleo.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Fedha, Mhandisi Mshamu Ally Munde, aliyekuwa mgeni rasmi akimwakilisha Waziri wa Fedha, Balozi Hamisi Mussa Omar, amesema takwimu rasmi ni nyenzo muhimu katika kutambua mafanikio yaliyofikiwa pamoja na maeneo yanayohitaji kupewa kipaumbele katika utoaji wa huduma kwa wananchi.

Akitolea mfano wa sekta ya afya, amesema takwimu zinaonesha kuwa asilimia 68 ya vituo vya kutolea huduma za afya vinapata huduma za msingi za maji ya kunywa, huku asilimia 80 vikipata huduma za msingi za usafi wa vyoo na mazingira, hali inayosaidia Serikali kutambua hali halisi na kupanga hatua za kuboresha huduma hizo.

Ripoti ya Anwary Shabani.