Dodoma FM

Tahadhari za usalama zaelekezwa kwa wazazi kipindi cha likizo

16 November 2026, 16:56

Picha ni watoto wakiwa nyumbani wakati wa likizo. Picha na Mwananchi.

Wazazi na walezi wametakiwa kuongeza uangalizi na kuchukua tahadhari za kiusalama kwa watoto katika kipindi hiki cha likizo na sikukuu za mwisho wa mwaka, ili kuzuia matukio ya watoto kupotea, kudhurika au kukumbwa na vitendo vya uhalifu.

Na Mwandishi wetu.

Wito huo umetolewa leo, Novemba 16, 2026, na Inspekta Nungwana Francis kutoka Kituo cha Polisi Kata ya Ipagala jijini Dodoma, alipokuwa akizungumza na chombo kimoja cha habari jijini humo, akisisitiza umuhimu wa wazazi kuhakikisha watoto wanapata uangalizi wa karibu wanapokuwa nyumbani, wanapocheza au wanapotembelea maeneo mbalimbali ya starehe.

Amesema wazazi na walezi wanapaswa kuepuka kuwaacha watoto katika mazingira yasiyo salama bila uangalizi, huku akiwashauri kuweka namba za simu za wazazi au walezi kwenye mifuko ya watoto ili kurahisisha mawasiliano endapo watapotea.

Ameeleza kuwa hatua hiyo itasaidia watu watakaokutana na watoto waliopotea kuwasiliana kwa haraka na familia zao, hivyo kurahisisha jitihada za kuwaunganisha tena na wazazi au walezi wao.

Sauti ya Inspekta Nungwana Francis kutoka Kituo cha Polisi Kata ya Ipagala jijini Dodoma.

Aidha, amesisitiza umuhimu wa wazazi kufuatilia mienendo ya watoto wao, kujua maeneo wanayokwenda kucheza pamoja na watu wanaoshirikiana nao, akibainisha kuwa usalama na ulinzi wa watoto ni jukumu la pamoja linalohitaji ushirikiano kati ya wazazi, walezi na jamii kwa ujumla.