Kituo cha afya Ihumwa kupunguza changamoto za huduma za afya
4 November 2026, 17:32

Kwa muda mrefu, ukosefu wa kituo cha afya umekuwa changamoto kwa wakazi wa Ihumwa, hususan wanawake wajawazito wanaohitaji huduma za dharura wakati wa kujifungua. Baadhi yao hulazimika kutafuta usafiri wa magari binafsi ili kufika Hospitali ya Mkoa wa Makole au Hospitali ya Rufaa ya General, hali inayowaongezea gharama za matibabu na usafiri.
Na Victory Chigwada.
Wananchi wa Kata ya Ihumwa jijini Dodoma wameeleza matumaini yao ya kupata nafuu ya huduma za afya kufuatia ujenzi wa kituo cha afya katika kata hiyo, wakisema kukamilika kwake kutapunguza adha ya kutegemea zahanati moja inayohudumia mitaa mitatu mikubwa.
Wananchi hao wamesema kukamilika kwa kituo hicho kutakuwa suluhisho la changamoto hiyo kwa kuwa kutarahisisha upatikanaji wa huduma za afya karibu na makazi yao na kupunguza gharama zinazotokana na kusafiri umbali mrefu kutafuta matibabu.
Akizungumzia ujenzi huo, Mwenyekiti wa Maendeleo wa Kata ya Ihumwa, Edward Magawa, ameishukuru Ofisi ya Mkurugenzi pamoja na Serikali Kuu kwa kuendelea kuweka kipaumbele katika kutatua changamoto zinazowakabili wananchi, ikiwemo upatikanaji wa huduma za afya.
Amesema ujenzi wa kituo hicho umefikia hatua za mwisho na unatarajiwa kukamilika ifikapo mwezi Desemba mwaka huu, hatua itakayokuwa na manufaa makubwa kwa wakazi wa kata hiyo.
Ikumbukwe kuwa ujenzi wa kituo hicho cha afya unafungamana na mradi wa ujenzi wa barabara ya mzunguko unaosimamiwa na Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), ukiwa na gharama ya shilingi bilioni 2.36 na kufikia zaidi ya asilimia 90 ya utekelezaji.