Upungufu wa dawa, gharama za huduma za afya zawakumba wananchi itiso
25 November 2026, 16:55

Akina mama wajawazito katika Kijiji cha Itiso, Wilaya ya Chamwino mkoani Dodoma, wamelalamikia gharama za huduma za afya wanazokutana nazo wanapokwenda kuanza kliniki na kupata huduma nyingine za uzazi, wakieleza kuwa hali hiyo inawaongezea mzigo wa kifedha.
Na Victory Chigwada.
Wakizungumza na Dodoma FM, baadhi ya wajawazito hao wamesema wamekuwa wakitozwa fedha kwa ajili ya vipimo wanapohudhuria kliniki, pamoja na gharama nyingine wanapokwenda kujifungua, hali wanayoieleza kuwa inatofautiana na taarifa wanazozisikia kuhusu huduma za afya zinazotolewa bila malipo kwa wajawazito na watoto walio chini ya umri wa miaka mitano.
Wamesema licha ya matarajio yao ya kupata huduma bila malipo, wamekuwa wakikumbana na gharama wanapofika katika zahanati ya kata na hospitali ya wilaya kwa ajili ya matibabu, huku wakiiomba Serikali na mamlaka husika kufuatilia hali hiyo ili kuhakikisha wanapata huduma kwa mujibu wa taratibu zilizowekwa.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Itiso, Bw. Halifa Punta, amekiri kuwepo kwa changamoto ya gharama za huduma za afya kwa wajawazito wanapokwenda kupata matibabu katika hospitali ya wilaya, akieleza kuwa suala hilo linahitaji kufanyiwa kazi ili kupunguza adha wanayokutana nayo wananchi.
Aidha, amesema changamoto nyingine inayowakabili wananchi ni upungufu wa dawa katika zahanati na hospitali ya wilaya, hali inayowalazimu baadhi ya wagonjwa kununua dawa katika maduka binafsi, huku akihimiza mamlaka husika kuboresha upatikanaji wa dawa na huduma za afya katika vituo hivyo.