Wazazi watakiwa kuongeza ulinzi wa watoto wakati wa likizo
19 November 2026, 16:34

Wazazi na walezi wanakumbushwa kuwa jukumu la kuwalinda watoto dhidi ya majanga ya mvua si la mamlaka pekee, bali linaanzia katika ngazi ya familia kwa kuhakikisha watoto wanapata uangalizi wa karibu na kuepuka maeneo yote yanayoweza kuhatarisha usalama na maisha yao.
Na Anwary Shabani.
Wazazi na walezi mkoani Dodoma wametakiwa kuongeza uangalizi kwa watoto wao katika kipindi hiki cha likizo, kwa kuhakikisha wanawazuia kucheza karibu na vyanzo vya maji, madimbwi na maeneo mengine yanayoweza kukusanya maji, kufuatia tahadhari ya mvua za El Niño zinazoendelea kutolewa.
Wakizungumza jijini Dodoma, baadhi ya wazazi wamesema ni muhimu kwa wazazi kutenga muda wa kutosha kukaa na watoto wao na kuwafuatilia mienendo yao, ili kuwazuia kwenda kucheza katika maeneo hatarishi yanayoweza kusababisha ajali na hata kupoteza maisha.
Wito huo umetolewa pia na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule, aliyewataka wazazi na walezi kushiriki kikamilifu katika kuwalinda watoto dhidi ya athari zinazoweza kujitokeza wakati wa mvua hizo.
Senyamule ametoa wito huo katika Kikao Kazi kilichowakutanisha na Wakuu wa Wilaya, Wakurugenzi pamoja na baadhi ya watendaji wa Mkoa wa Dodoma, kilicholenga kujadili ajenda mbalimbali za maendeleo, ikiwemo taarifa ya utekelezaji wa maandalizi ya kukabiliana na athari za mvua za El Niño katika kipindi cha likizo.