Wanaume wahimizwa kuimarisha ulinzi kwa wanawake na watoto
26 November 2026, 16:58

Vitendo vya ukatili na unyanyasaji dhidi ya wanawake na watoto vimeendelea kuwa changamoto katika jamii, huku wanaume wakihimizwa kutumia nafasi zao kama wazazi, walezi na walinzi kushiriki kikamilifu katika mapambano ya kutokomeza vitendo hivyo na kujenga jamii yenye usalama na haki kwa wote.
Na Daniel Njau.
Baadhi ya wananchi wamesema wanaume wana nafasi muhimu katika kuimarisha ulinzi wa wanawake na watoto, kwa kushiriki katika malezi, kutoa elimu na kushirikiana na jamii kuhakikisha makundi hayo yanaishi katika mazingira salama yasiyo na ukatili.
Mlezi wa kituo cha watoto cha Esses Children, Bi. Lea Matalali, amesema ushiriki wa wanaume katika mapambano dhidi ya ukatili wa kijinsia ni muhimu, akibainisha kuwa baadhi yao wamekuwa wakiacha jukumu la malezi kwa wanawake pekee, badala ya kushiriki kikamilifu katika kuwalea na kuwalinda watoto wao.
Amesema watoto wanaokulia katika mazingira yenye ukatili na unyanyasaji wanaweza kupata athari za kisaikolojia, ambazo huathiri ukuaji na mwenendo wao, huku baadhi yao wakihatarisha kujenga tabia zinazofanana na mazingira waliyokulia, hivyo kusisitiza umuhimu wa malezi yenye upendo, usalama na heshima.
Aidha, amesisitiza kuwa jukumu la kumlinda mtoto na kumpatia malezi bora halipaswi kuachiwa mzazi mmoja, bali linahitaji ushirikiano wa wazazi wote wawili, walezi na jamii kwa ujumla, ili kujenga kizazi kinachozingatia haki, heshima na usalama wa wengine na kuchangia kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake na watoto.