DUWASA yaendelea kutafuta suluhisho la changamoto ya maji Bahi
9 October 2026, 10:24

Baadhi ya wananchi wilaya ya Bahi wamesema pamoja na kuona mabadiliko katika upatikanaji wa maji, bado wanakabiliwa na changamoto ya maji yenye chumvi nyingi, hali inayosababisha usumbufu katika matumizi ya nyumbani.
Na Anwary Shabani.
Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dodoma (DUWASA) inaendelea kutekeleza miradi ya muda mfupi na mrefu inayolenga kuongeza upatikanaji wa maji na kupunguza changamoto ya maji yenye chumvi katika Kanda ya Bahi, mkoani Dodoma, huku wananchi wakiendelea kutarajia huduma ya maji safi na salama.
Akizungumza wakati wa maadhimisho ya Wiki ya Huduma kwa Wateja yanayofanyika kuanzia Oktoba tano hadi tisa mwaka huu, Mkurugenzi wa Kitengo cha Ununuzi na Ugavi wa DUWASA, Alex Mahere, amesema mamlaka hiyo inaendelea kuweka mikakati ya kuboresha huduma ya maji ili kuhakikisha wateja wanapata huduma bora na inayokidhi mahitaji yao.

Kwa upande wake, Meneja wa Kanda ya DUWASA Bahi, Winfrida Masawe, amesema wiki hiyo ni fursa kwa mamlaka hiyo kusikiliza maoni ya wananchi, kupokea malalamiko na kutafuta ufumbuzi wa changamoto zinazowakabili watumiaji wa maji katika eneo hilo
Amesema changamoto kubwa zinazojitokeza ni maji kuwa na chumvi pamoja na upungufu wa maji wakati wa kiangazi, huku akieleza kuwa utekelezaji wa miradi inayoendelea unalenga kuboresha upatikanaji na ubora wa huduma hiyo.

Akizungumzia hali hiyo, Samson Kidiala, mkazi wa Bahi, amesema maji yamekuwa yakipatikana kwa muda mfupi ikilinganishwa na ilivyokuwa awali, huku maji yenye chumvi yakiathiri nguo na kuongeza matumizi ya mafuta ya kupaka mwilini baada ya kuoga.
Hivyo, utekelezaji wa miradi hiyo na juhudi za DUWASA kusikiliza malalamiko ya wateja vinatajwa kuwa hatua muhimu katika kutafuta suluhisho la changamoto ya maji Bahi, huku wananchi wakisubiri kuona matokeo yatakayoboresha upatikanaji wa maji ya kutosha, safi na salama kwa matumizi ya kila siku.