Wakulima watakiwa kuzingatia utabiri wa hali ya hewa
20 October 2026, 16:39

Wito huo unakuja wakati wakulima wakijiandaa kuanza msimu mpya wa kilimo, ambapo matumizi ya taarifa sahihi za hali ya hewa na ushauri wa wataalamu yanatarajiwa kuwa na mchango muhimu katika kuimarisha uzalishaji wa chakula na kuinua uchumi wa kaya.
Na Stephen Noel.
Wakulima wametakiwa kuzingatia taarifa za utabiri wa hali ya hewa zinazotolewa na wataalamu wa hali ya hewa ili kupanga vizuri shughuli zao za kilimo na kuongeza uzalishaji wa mazao katika msimu mpya wa kilimo.
Wakiongea na Dodoma Fm Kwa mahojiano maalumu Elisha Maulid na Rayson Mosha, ambao wameeleza umuhimu wa wakulima kupata na kufuatilia taarifa sahihi za hali ya hewa kabla na wakati wa kuanza shughuli za kilimo.
Wamesema kuwa kuzingatia taarifa hizo kutawasaidia wakulima kufanya maamuzi sahihi kuhusu muda wa kuandaa mashamba, kupanda mbegu na kuchagua mazao yanayoweza kustahimili mazingira ya msimu husika.
Aidha, wamesisitiza kuwa wakulima wanapaswa kuepuka kutegemea mazoea ya misimu iliyopita pekee, badala yake kutumia taarifa za kitaalamu katika kupanga shughuli zao ili kupunguza uwezekano wa kupata hasara inayoweza kusababishwa na mabadiliko ya hali ya hewa.
Kwa upande wake, Afisa Kilimo, Leah Mlunguja, amewataka wananchi kuzingatia maelekezo na ushauri unaotolewa na wataalamu wa kilimo pamoja na kufuatilia taarifa rasmi za utabiri wa hali ya hewa.
Mlunguja amesema kuwa matumizi ya taarifa sahihi za kitaalamu ni muhimu katika kuwawezesha wakulima kupanga shughuli zao kwa wakati, kuchagua mbinu bora za uzalishaji na kukabiliana na changamoto zinazoweza kujitokeza katika msimu wa kilimo.
Ameongeza kuwa wakulima wanapaswa kuendelea kushirikiana na maafisa ugani ili kupata elimu kuhusu mbinu bora za kilimo, uchaguzi wa mbegu bora na namna ya kutunza mazao kulingana na hali ya hewa inayotarajiwa.