Dodoma FM

Korongo la Chinyasungwi tishio msimu wa mvua Chilwana

6 November 2026, 12:32

Msimu wa mvua mawasiliano hukatika kutokana na korongo hilo kujaa maji.Picha na Dodoma fm.

Korongo hilo linatenganisha vijiji na vitongoji kadhaa ambavyo vina muingiliano wa shughuli mbalimbali ikiwemo kilimo na biashara.

Na Victor Chigwada.

Wakazi wa kitongoji cha Mbelezungu B wilayani Chamwino wameomba kujengewa kivuko katika Korongo la Kinyasungwi kuelekea msimu wa mvua ili kuepusha madhara yanayoweza kuwapata wanapovuka korongo hilo.

Wakiongea na taswira ya habari wakazi hao wamesema adha ya ikosefu wa kivuko katika eneo hilo imedumu kwa muda mrefu na inapo fika msimu wa mvua mawasiliano hukatika kutokana na korongo hilo kujaa maji na kupelekea wananchi kushindwa kuvuka kwenda upande mwingine.

Aidha wananchi hao wameiomba serikali kuwajengea kivuko kwani kujaa maji kwa korongo hilo hukwamisha shuguli za kilimo pia kutokana na baadhi ya wananchi kushindwa kuvuka kwenda shambani wakihofia kusombwa na maji.

George Isaya mwenyekiti wa Kijiji cha Mbelezungu amesema  Kwa misimu miwili wamekumbana na changamoto ya watu kuchukuliwa na maji ya korongo na kupoteza maisha kutokana na ukosefu wa kivuko katika korongo hilo.

Amesema Korongo hilo linatenganisha vijiji na vitongoji kadhaa ambavyo vina muingiliano wa shughuli mbalimbali ikiwemo kilimo na biashara hivyo kukosekana kwa kivuko kumekuwa kukipelekea shughuli hizo kukwama msimu wa mvua.

Ripoti ya Victor Chigwada.