Dodoma FM

Ukosefu wa zahanati wapelekea huduma za klinik kutolewa chini ya mti Ilolo

28 October 2026, 17:51

Ukosefu wa zahanati ya karibu umepelekea huduma za cliniki kufanyika chini ya mti katika kitongoji hicho.Picha na global.

Ujenzi wa zahanati ya  Ilolo unafanyika  kwa nguvu za wananchi.

Na Victor Chigwada.

Wakazi wa kitongoji cha Ilolo kata ya Ihumwa wamelalamika kutembea umbali mrefu ili kupata huduma ya afya katika Zahati ya kata.

Wananchi hao wamesema licha ya kutumia nguvu kazi za wananchi kuhakikisha wanaanzisha ujenzi wa zahanati lakini bado hakuna matumaini ya kukamilika kwa ujenzi huo.

Ukosefu wa zahanati ya karibu umepelekea huduma za cliniki kufanyika chini ya mti katika kitongoji hicho kuwapima akinamama wajawazito na watoto hali ambayo si rafiki hasa msimu wa mvua.

Hata hivyo taswira ya habari imezungumza na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Dodoma Jiji Bw. Fredrick Segamiko ambaye emekiri kuwa  ujenzi wa zahanati ya  Ilolo unafanyika  Kwa nguvu za wananchi na walifika kufanya tathimini ya kumalizia ujenzi huo na kupata jumla ya Milioni arobaini na sita na tayari zilisha wekwa kwenye akaunti yao ya maendeleo ya kata.

Segamiko amekiri uwepo wa fedha za utekelezaji wa miradi mbalimbali lakini changamoto kwa baadhi ya Kata kusua sua na matumizi au kubadili matumizi na kutoa wito Kwa uongozi wa Kata ya Ihumwa kukamilisha ujenzi wa zahanati hiyo ya Ilolo .

Ripoti ya Victor Chigwada.