Vijana wahimizwa kutumia vipaji na talanta kujikwamua kiuchumi
1 September 2026, 16:25

Vijana wameshauriwa kujitangaza kupitia vipaji na talanta zao, kufanya kazi kwa bidii na kujiwekea malengo yanayotekelezeka, huku wakitumia maarifa na uzoefu wa waliofanikiwa kama njia ya kujenga fursa za kiuchumi na kupunguza utegemezi wa ajira.
Na Daniel Njau.
Vijana wametakiwa kujiamini, kutumia vipaji na talanta walizonazo pamoja na kuweka malengo katika kile wanachokifanya ili kujikwamua kiuchumi badala ya kutegemea ajira pekee.
Wananchi wamesema ni muhimu vijana kutambua uwezo walionao, kujifunza kutoka kwa watu waliofanikiwa na kutumia fursa zilizopo kujiajiri na kufikia malengo yao ya maisha.
Kwa upande wake,Bw Hamisi Kasogo kutoka mashirika yasiyo ya kiserikali (NGOs) amesema mfumo wa elimu umekuwa ukimwandaa zaidi kijana kusoma na hatimaye kutafuta ajira, hali inayowafanya baadhi yao kushindwa kutumia maarifa waliyopata darasani katika vitendo kwa ajili ya kujiajiri.