Shekimweri atatua mgogoro wa wafanyabiashara wa soko la umonga
25 May 2026, 16:42

Hatua hiyo ni sehemu ya jitihada za serikali za kuendelea kuimarisha masoko na kuboresha mazingira ya biashara kwa wananchi.
Na Mariam Kasawa.
Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Alhaj Jabir Shekimweri amehudhuria mkutano wa wazi uliowakutanisha wafanyabiashara wa Soko la Umonga waliohamishwa kutoka Soko la Rehema Nchimbi kupisha shughuli za eneo la Bunge.
Mkutano huo uliwakutanisha wafanyabiashara, viongozi wa soko pamoja na viongozi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma ukiwa na lengo la kujadili na kuweka sawa masuala mbalimbali yanayohusu urasimu wa mikataba, upangaji wa maeneo ya biashara pamoja na kuondoa changamoto zinazowakwamisha wafanyabiashara kurejea katika shughuli zao katika soko hilo.
Akizungumza katika mkutano huo, Alhaj Shekimweri aliwataka viongozi wa Soko la Umonga pamoja na viongozi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma kuhakikisha wanasimamia kwa haki na uadilifu mchakato mzima wa ugawaji wa maeneo ili kuondoa migogoro miongoni mwa wafanyabiashara.

Aidha, alisisitiza kuwa wafanyabiashara wote wana haki ya kupata maeneo katika soko hilo, ikiwemo waliokuwa na vizimba hapo awali waliokuwa wamepanga pamoja na wengine watakaohitaji maeneo endapo nafasi zitakuwepo.
Pia, alitoa agizo kuwa wafanyabiashara wasinyimwe maeneo yao kwa sababu ya kutokuwa na leseni za biashara, akieleza kuwa suala hilo linaweza kushughulikiwa wakati wafanyabiashara wakirejea katika maeneo yao waliyopangiwa.
Kwa upande wake, mfanyabiashara wa Soko la Umonga, Baraka Donald aliishukuru serikali kwa kuandaa mkutano huo ambao umeleta suluhu ya changamoto zilizokuwa zikikwamisha mchakato wa uhamiaji wa wafanyabiashara hao.