Teknolojia ya robots kukuza uchumi wa kidijitali
31 July 2026, 17:00

Wasichana wakipata elimu kuhusu matumizi ya teknolojia ya Robots katika kukuza uchumi Tanzania. Picha na Mtandao
Mafunzo hayo ni matokeo ya dhamira ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya kuwawezesha watumishi wa umma kumudu teknolojia zinazoibukia, akieleza kuwa sasa ana uwezo mkubwa zaidi wa kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi kutokana na maarifa aliyoyapata.
Na Anwary Shabani.
Imeelezwa kuwa elimu ya Robots kupitia Mradi wa Tanzania ya Kidijitali itasaidia kuongeza ushiriki wa wasichana katika taaluma za TEHAMA na kuharakisha matumizi ya teknolojia za kisasa katika sekta mbalimbali nchini.
Hayo yamesemwa na Muhandisi Mwandamizi wa Mawasiliano kutoka Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF), Brian Kaduma, ambapo amesema elimu hiyo aliyo ipata itakuwa msaada wa kuharakisha matumizi ya teknolojia za kisasa katika sekta mbalimbali za uzalishaji nchini.
Akizungumza jijini Dodoma, Kaduma amesema ujuzi huo ataupeleka moja kwa moja katika utekelezaji wa programu ya “Msichana katika TEHAMA” inayoratibiwa na UCSAF, kwa kuwapatia wanafunzi wa kidato cha tatu maarifa ya msingi ya Robotics ili kuwajengea hamasa ya kujiunga na taaluma za teknolojia na kuwa wataalamu wa baadaye.
Aidha, ametoa wito kwa wadau mbalimbali kushirikiana na Serikali kuendelea kuwekeza katika elimu ya teknolojia kwa watumishi wa umma na wananchi kwa ujumla, akisema hatua hiyo itachangia kujenga jamii yenye ujuzi wa kidijitali na kuongeza ushindani wa Tanzania katika uchumi wa kisasa.