Dodoma FM

Malezi huchangia watoto wa kiume kushindwa kuripoti ukatili

16 June 2026, 17:17

Wazazi na walezi hawawajengei watoto wa kiume uwezo wa kujieleza na kutoa taarifa wanapokumbana na vitendo vya ukatili,Picha na Mtandao.

Kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na Sheria ya Mtoto ya mwaka 2009, kila mtoto ana haki ya kulindwa dhidi ya aina zote za ukatili, unyanyasaji na ubaguzi, huku jamii ikihimizwa kushiriki kikamilifu katika kuhakikisha mazingira salama kwa watoto wa kike na wa kiume.

Na Elizabeth Mwailunga.

Baadhi ya watoto wa kiume hushindwa kuwa wazi na kuripoti vitendo vya ukatili wanavyofanyiwa kutokana na malezi na makuzi wanayopata wakiwa wadogo.

Hayo yameelezwa na Afisa wa Dawati la Jinsia na Watoto Mkoa wa Dodoma, Michael Mkinda, alipokuwa akizungumza na Taswira ya Habari.

Amesema baadhi ya wazazi na walezi hawawajengei watoto wa kiume uwezo wa kujieleza na kutoa taarifa wanapokumbana na vitendo vya ukatili, jambo ambalo huendelea kuwaathiri hata wanapokuwa watu wazima.

Sauti ya Michael Mkinda,

Mkinda amesema malezi ndiyo msingi wa kumjenga mtoto katika maadili, mitazamo na uwezo wa kukabiliana na changamoto mbalimbali za maisha, hivyo ni muhimu wazazi kuwafundisha watoto wao kusema ukweli na kutafuta msaada wanapokutana na vitendo vya ukatili.

Akizungumzia namna Dawati la Jinsia na Watoto linavyowahudumia wanaume wanaoripoti ukatili, amesema dawati hilo linazingatia usiri wa taarifa na ulinzi wa faragha ya wahanga wote wanaojitokeza kutoa taarifa.

Sauti ya Michael Mkinda,

Aidha, ametoa wito kwa wazazi na walezi kuwajenga watoto wao katika misingi ya kujiamini, kushiriki katika maamuzi na kuwa na uwezo wa kueleza changamoto wanazokutana nazo, ili wawe tayari kuripoti vitendo vya ukatili na kupata msaada kwa wakati.

Sauti ya Michael Mkinda,